Monzinzi atetewa Azam wakiipania Yanga

Unguja. Azam FC jana Jumapili usiku walitinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi lakini uongozi wa klabu hiyo umeonekana kumkingia kifua straika wao mpya Mpiana Monzinzi kuwa apewe muda zaidi.

Azam ilifuzu hatua hiyo baada ya kuifunga Malindi bao 1-0 lililofungwa na Agrey Morris kwa mkwaju wa penati hivyo leo Jumatatu saa 10:00 jioni watacheza na Yanga huku wakitamba kupata ushindi dhidi ya Wanajangwani hao.

Monzinzi katika mashindano haya amefunga bao moja ambapo jana alishindwa kuonyesha makeke yake huku Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Popat akisema anatakiwa muda zaidi wa kuonyesha uwezo wake.

"Nadhani hatuwezi kumhukumu kwa mechi mbili alizocheza ingawa mechi ya kwanza alifunga, tumpe muda zaidi hata mechi tano ndipo tunaweza kumhukumu kama hatafunga ila naamini ni mchezaji mzuri na hali kama hii huwa inatokea kwa kila mchezaji.

"Kikubwa tumeingia nusu fainali ambapo tunatakiwa kupambana kutinga fainali maana lengo letu ni kutwaa ubingwa japokuwa mashindano ya msimu huu ni magumu na kila timu imejiandaa vizuri," alisema Popat na kuongeza kuwa

"Tunacheza na Yanga lakini sio timu ya kuihofia, kama nilivyoeleza kila timu iliyoshiriki mashindano haya ilikuwa na upinzani kikubwa ni kujipanga, naamini tutafanya vizuri na kutinga fainali," alisema Popat

Leo katika hatua hiyo ya nusu fainali, Yanga wataanza kucheza na Azam saa 10 jioni wakati nusu fainali ya pili itachezwa usiku ambapo Simba itaikaribisha Namungo, mechi zote zitachezwa Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika keshokutwa Jumatano Januari 13.