Aussems: Nipeni Simba yangu

PATRICK Aussems maarufu kama ‘Uchebe’ aliyekuwa kocha wa Simba ametamka kwamba yuko tayari kurejea Msimbazi kuchukua nafasi ya Sven Vandenbroeck huku akitamba kuwa kikosi cha sasa Simba kinaweza kutisha kimataifa kama kikitumika vizuri.

Ametamba kwamba akiiongoza Simba hii yenye Luis Jose, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na wengine wazuri ana uwezo wa kuweka kibindoni pointi 10 na kwenda robo fainali.

Licha ya kufanya usiri mkubwa katika mchakato wa kumsaka kocha mpya, Mwanaspoti ambalo lilikuwa la kwanza kukupa habari ya Sven, kuwaacha Simba pasipo wao kutarajia, linafahamu kwamba hadi sasa uongozi wa Simba umebaki na majina matano tu ya makocha baada ya kufanya mchujo katika wasifu (CV) wa makocha 100 tofauti kutoka ndani na nje ya Afrika.

Aussems ameibuka na kuwashtua mabosi hao wa Simba kuwa yuko tayari kurejea ili aendeleze pale alikoishia ambako ni kuwafikisha katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Aussems alisema: “Nipo tayari kurudi tena kuifundisha timu hiyo kwani imekuwa na kikosi bora zaidi ya misimu miwili nyuma wakati nawafundisha. Nipo tayari kurudi kama nitapokea simu kutoka kwa kiongozi wa Simba, lakini wakati huu nipo katika tafakari ya maamuzi kwani nina ofa kutoka katika timu mbalimbali za huko Afrika.”

Kocha huyo mwenye uzoefu na Soka la Afrika na ambaye Mwanaspoti linajua kabla ya kuajiriwa kwa George Lwandamina huko Azam walimtaka lakini baadaye wakamkaushia aliongeza kuwa: “Simba nimeishi nao vizuri na milango ipo wazi na nawapa nafasi kuliko timu nyingine yoyote ambayo inanihitaji. Simu ambayo nimepokea ni ya kiongozi mmoja mkubwa kutoka Azam kuona namna gani naweza kuja huko ila hatukufika mbali na hatukuendelea zaidi katika maongezi haya.”

Aussems alisema kikosi cha Simba msimu huu ni bora kuliko wakati anafundisha na wanaweza kufanya vizuri si katika Ligi Kuu Bara na mashindano ya ndani bali hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema ukiangalia kundi la Simba kimataifa kuna Al Ahly na AS Vita ambao walikutana nao msimu waliofika robo fainali wakati anafundisha kwa maana hiyo wanaweza kuwafunga tena kwavile anawajua na kuna mambo alijifunza ndani na nje ya uwanja.

“Kikosi cha Simba kinaweza kufanya vizuri dhidi ya Al Ahly na AS Vita na wakapata matokeo mazuri dhidi ya timu hizo lakini El Merreikh siwafahamu zaidi ila timu kutoka ukanda wa Sudan mara nyingi si za kutisha,” alisema Aussems ambaye hivi karibuni alisaini dili na Black Leopards ya Sauzi lakini aliachana nayo mwezi mmoja baadaye kwa kupoteza mechi tatu mfululizo.

“Kama Simba wataweza kuwa na silaha yao ya kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kama wakati nafundisha na wakawa na nidhamu ugenini dhidi ya El Merreikh wanaweza kumaliza kundi kwa kufuzu robo fainali wakiwa na pointi kumi.

“Sijafanya mawasiliano yoyote na Sven, ila kimsingi kuifundisha timu na ikafika hatua ya timu 16, bora ni sifa kubwa kwa kocha ambaye amepata mafanikio katika mashindano ya nyumbani na si jambo la kushangaza kuona amepata ofa kubwa kutoka katika nchi nyingine.

“Kikosi cha Simba ukiangalia mchezaji mmoja mmoja katika uwezo wake binafsi umeimarika na kuwa juu zaidi jambo ambao linampa uhakika wa kocha kufanya vizuri katika kila mechi.

“Kwa maana hiyo nipo tayari kurudi Simba kama watanifuata na milango ipo wazi kwani ni miongoni mwa timu ambayo falsafa yangu ya kucheza soka la kushambulia na kuvutia mashabiki na wachezaji wake wana sifa nyingi za kuelewa na kuutumia kwa haraka.”