Mogella: Chama, Mayele wataamua

Muktasari:

  • Simba itavaana na Horoya leo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Yanga kushuka uwanjani Jumapili kumalizana na US Monastir na ushindi kwa timu hizo utazivusha makundi na kwenda robo fainali na Mogella alisema mastaa hao ndio watakaoamua mechi hizo.

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika na Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella amesema Clatous Chama na Fiston Mayele ndio walioshikilia tiketi za robo fainali za CAF kwa timu hizo kongwe kwa mechi zitakazopigwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba itavaana na Horoya leo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Yanga kushuka uwanjani Jumapili kumalizana na US Monastir na ushindi kwa timu hizo utazivusha makundi na kwenda robo fainali na Mogella alisema mastaa hao ndio watakaoamua mechi hizo.

Mogella aliyepachikwa jina la Golden Boy mwaka 1981 kutokana na ubora  wake wa kufunga mabao aliwachambua washambuliaji hao na kuona wanaweza kuzibeba timu zao kama tu watakuwa na utulivu.

"Chama anaweza akaumaliza huu mchezo kwa sababu kinachohitajika ni matokeo naye ana ubora mkubwa wa kutengeneza nafasi kwahiyo kama akiamka vizuri na atakuwa kwenye kiwango chake basi watamaliza mechi mapema," alisema Mogella na kuongeza;

"Mechi hizi unatakiwa kutumia kila nafasi kwa sababu upatikanaji wake ni mdogo kwahiyo waheshimu kila ambacho kinapatikana kwa wakati sahihi ili waweze kusonga mbele."
Kwa upande wa Mayele alisema anatakiwa aache ubinafsi wa kutaka afunge yeye tu kwa sababu mpira wa sasa umebadilika lakini kinachohitajika ni matokeo mazuri kwa timu.

"Mayele ni mshambuliaji mzuri lakini changamoto kubwa huwa ni mchoyo, kuna muda hayupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga lakini analazimisha wakati mwenzake yupo sehemu sahihi. Unajua straika ukiwa unakaa kwenye nafasi nzuri basi  ni rahisi kufunga, kuna muda unaona hapa siwezi kufunga haupaswi kulazimisha bali unamuangalia nani ambaye yupo sehemu nzuri ya kufunga," alisema.

Chama amefunga bao moja katika makundi hadi sasa, huku Mayele akifunga mabao mawili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, mbali na mabao saba aliyofunga hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa