Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mnyama alifia hapa kwa Mkapa

HUKO mtaani mambo yametulia baada ya mechi ya watani kupigwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na Yanga kumaliza ubishi kwa kuwanyoosha Simba kwa bao 1-0 katika pambano kali la Ngao ya Jamii.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wachache kulinganisha na Kariakoo Derby nyingine, Yanga ilipata ushindi wake kwa bao tamu lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake, Fiston Mayele aliyemalizia pasi nzuri ya Farid Mussa dakika ya 12 tu ya mchezo huo uliochezeshwa na Ramadhan Kayoko.

Ubora na ufanisi wa safu ya kiungo ya Yanga ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa ushindi wao.

Viungo wa Yanga waliwapoteza wenzao wa Simba kwa kuwanyima uhuru wa kumiliki mpira, kutengeneza nafasi na kupenya kupitia katikati kulisogelea lango lao walipokuwa wanashambulia.

Hilo liliwalazimisha Simba kubadili staili yao ya kiuchezaji na kutumia zaidi mipira ya juu hasa ile ya kutokea pembeni ambayo iliokolewa vizuri na mabeki na viungo wa Yanga

Ugumu kwa Simba uliongezeka zaidi pale wapinzani wao walipokuwa na mpira, kwani viungo hao ambao walikuwa ni Khalid Aucho, Yannick Bangala na Feisal Salum ‘Fei Toto’ walikuwa wepesi kufanya uamuzi wa haraka na kuisukuma timu mbele, wakitoa pia usaidizi kwa mastraika wao waliposhambulia

Ubora wa watatu hao uliwafanya viungo wa chini na mabeki wa Simba kupaniki na kucheza rafu zilizowafanya waonyeshwe kadi na mwamuzi Kayoko aliyechezesha vyema.

Mbali na kiungo, Yanga pia walikuwa imara zaidi kwenye eneo la ulinzi kwani, nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job na mabeki wa pembeni Djuma Shaban na Kibwana Shomary walikaba na kupandisha mashambulizi, huku wakipigwa tafu na kina Bangala na Aucho ambao walikuwa imara zaidi na kuwavutia mashabiki wa kutokaa na kiwango chao

.

PUPA ILIPOANZA SIMBA

Licha ya kutocheza vizuri, Simba ilitengeneza nafasi kadhaa ambazo kama nyota wake wangekuwa makini na utulivu mbele ya eneo la hatari la adui, ingetosha kuwapa bao au hata mabao. Ilikuwa ni siku mbaya kwa Chris Mugalu aliyepoteza nafasi mbili za wazi mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kushindwa kuunganisha krosi ya Mohamed Hussein na nyingine kupiga shuti lililotoka nje alipokuwa akiunganisha krosi ya Pape Sakho.

Wachezaji wa Simba walionekana kupoteza umakini na utulivu kutokana na kutangulia kufungwa bao la mapema jambo lililowafanya waonekane wakicheza wakiwa na presha kubwa, huku pengo la Clatous Chama na Luis Miquissone likionekana dhahiri kwenye mechi hiyo.

Simba haikuwa katika ubora wao wa kumiliki mpira na hata ilipokuwa na m,ipira walikuwa hawawezi kukaa nao kwa muda mrefu kabla hawajaporwa, tofauti na enzi za kina Chama na Luis waliokuwa wanaiendesha timu watakavyo na hasa inapokuwa mechi kubwa kama hii ya Kariakoo Derby.


DIARRA AONYESHA THAMANI YAKE

Kipa Djigui Diarra wa Yanga anaweza asizungumzwe na kutajwa sana lakini ni miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika ushindi na kiwango bora cha timu hiyo.

Nyota huyo kutoka Mali aliipanga vyema safu yake ya ulinzi na kuwasiliana nayo mara kwa mara na pia aliondosha hatari kadhaa zilizoelekezwa langoni mwake kwa ustadi mkubwa.

Kana kwamba haitoshi, uwezo wa kipa huyo kuichezesha timu kwa mipira yake mirefu ambayo ilifikia walengwa kwa usahihi, ulikuwa mwiba kwa Simba na ndiye aliyeanzisha mpira uliozaa bao pekee la ushindi kwa Yanga.


MASHABIKI KIDUCHU

Moja ya jambo la kushangaza katika mechi hiyo ni idadi ndogo ya mashabiki waliojitokeza uwanjani kulinganisha na mechi nyingine ambazo hukutanisha timu hizo mbili.

Viti vingi ya majukwaa ya Uwanja wa Benjamin Mkapa vilionekana kuwa vitupu na hivyo kuifanya mechi hiyo kuingia katika historia ya kuwa kati ya mechi za watani wa jadi zilizohudhuriwa na mashabiki wachache zaidi tangu uwanja huo ulipoanza kutumika.


 YANGA INA KIKOSI CHA MABINGWA

Tofauti na misimu minne iliyopita ambayo Yanga haikutwaa ubingwa kutokana na kuwa na kundi kubwa na wachezaji wasio wa daraja la juu, safari hii wanaonekana kuja kivingine.

Nyota 11 walioanza katika mchezo wa juzi, walicheza vyema kitimu lakini pale walipolazimika kuonyesha uwezo binafsi walifanya hivyo

Jambo zuri kwao kwenye benchi walikuwa na wachezaji wengine wa ambao walicheza vizuri pindi walipoingia.

Kiwango bora cha Farid Musa ambaye kwa muda mrefu alisotea benchi, ni ishara kwamba Yanga imebadilika na itakuwa washindani wakubwa wa Simba katika kuwania mataji msimu huu.


WASIKIE WADAU

Mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Said alisema Yanga walikuwa bora kimbinu.

“Simba waliingia katika mtego wa Yanga ambayo iliwaachia mara kadhaa kumiliki mpira huku ikiwazibia mianya na kuwapa mbinyo jambo ambalo walifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Mechi iliisha tangu kipindi cha kwanza na Simba walionekana kukosa mpango B,” alisema Jemedari.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema kuwa mchezo wa juzi unapaswa kuwa darasa kwa timu hiyo

“Ni matokeo ya mchezo naamini benchi la ufundi litatazama upungufu na kuufanyia kazi na timu itafanya vizuri katika michezo inayokuja mbele yake,” alisema Mgosi.