Mmarekani arithi mikoba ya Djuma Dodoma

BAADA ya uongozi wa timu ya Dodoma Jiji kuachana na benchi lake la ufundi lililokuwa chini ya Masoud Djuma, timu hiyo imemtangaza aliyekuwa kocha wa Coastal Union na Gwambina, Melis Medo kuchukua nafasi hiyo.
Medo ambaye anasifika kwa misimamo yake, ana kibarua cha kwanza cha timu hiyo kwenye mchezo wa ugenini, Jumapili wiki hii, wilayani Mbarali, timu yake itakapovaana na Ihefu SC kwenye uwanja wa Highland Estates.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 11 Jijini hapa  ilieleza kuwa Dodoma Jiji  wamefikia makubaliano na Medo kuwa kocha mkuu.

"Uongozi unawaomba mashabiki wetu na wapenda michezo kumpa ushirikiano wa kutosha kocha Medo katika kipindi chote atakachohudumu kama Mkuu wa benchi la ufundi," ilieleza taarifa hiyo.

Kocha huyo pia amepewa jukumu la kuchagua msaidizi wake ambaye atatangazwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kimkataba, huku kocha wa makipa pia atatangazwa baada ya uamuzi wa kocha na uongozi.

''Kocha tumempa uhuru wa kuchagua msaidizi wake naamini kabla ya kwenda Mbarali kama mambo yatakwenda sawa tutamtangaza, upande wa kocha wa makipa bado tupo kwenye majadiliano kwa pamoja'' alisema kiongozi wa timu hiyo.

Wakati huohuo, aliyekuwa kocha msaidizi wa Masoud Djuma, Muhammed Muya, amerudishwa ndani ya timu hiyo ambapo safari hii atakuwa na jukumu la kuhakikisha utimamu na ufiti wa wachezaji unakuwa na ufanisi.

Muya atashirikiana na Medo na msaidizi wake kuhakikisha timu hiyo inakuwa na uwezo wa kuhimili mechi tofauti, ambapo kwenye mechi za timu hiyo msimu huu, wachezaji walikuwa wanachoka isivyotarajiwa.