Mkwasa: Lazima tupambane kutafuta nne bora

Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amesema hafurahishwi na jinsi kikosi chake kisivyo na muendelezo mzuri wa ushindi kwenye Ligi Kuu Bara na atayatumia mapumziko mafupi ya ligi kufanya marekebisho kwa matatizo yote yanayosababisha jambo hilo  ili wakirejea wawe katika kiwango bora.
Mkwasa amekiri hawakuanza vizuri ligi msimu huu lakini baadae walikaa sawa na kucheza kwa kiwango kikubwa lakini siku za karibuni hawakuwa na mwendelezo wa ubora wao.
Amesema bado kikosi chake ni kizuri muhimu ni kuongeza upambani uwanjani ili kuhakikisha wanamaliza ligi katika nafasi nne za juu kama walivyojiwekea malengo.
"Kweli hatuna muendelezo mzuri kwenye ligi kwa sasa kwa sababu kun amuda tunashinda mechi moja halafu mbili zinazofuata tunapoteza jambo ambalo halifurahishi.
"Kipindi hiki cha mapumziko mafupi ya ligi tunatakiwa kuangalia wapi tunakosea ili kurekebisha na ligi ikirejea turudi kwenye ubora wetu kwa kuhakikisha tunashinda mechi zetu nyingi zilizobaki ili tumalize katika nafasi nne za juu," amesema Mkwasa.
Mkwasa amekiri Ligi imekuwa ngumu sana  kwani inaelekea ukingoni na kila timu inapambana kutimiza malengo waliyojiwekea.
"Sasa hivi kuna timu zinazopamba kujiokoa na janga la kushuka daraja, kuna zinazowania ubingwa na nafasi za juu hivyo imeifanya ligi kuwa ngumu sana na ili ushinde inatakiwa upambane hasa ," amesema Mkwasa.