Mkizingua viwanja vinafungiwa

BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imesisitiza kuendelea kuvipiga pini viwanja vyote ambavyo vitakuwa na matatizo kwa mujibu wa kanuni licha ya ligi kuendelea kupigwa kwa sasa.

Mpaka jana jumla ya viwanja vitano vilikuwa vimefungiwa ambavyo ni Kumbukumbu ya Karume uliopo Mara, Gwambina Complex wa Mwanza, Jamhuri Morogoro, Ushirika uliopo Moshi pamoja na Mabatini Mlandizi. Baada ya kufungiwa kutokana na sababu mbalimbali timu zilizoathirika na adha hiyo kama Mtibwa Sugar, Gwambina, Polisi Tanzania, Mwadui na Ruvu Shooting zilitakiwa kuchagua viwanja vipya kwa ajili ya michezo yao ya nyumbani.

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo aliyekiri kwa namna mambo yanavyojitokeza katika viwanja wakati ligi ishaanza na kubaini mapungufu wao wanachukua hatua.

“Uwanja muda mwingine unaweza kuharibika baada ya kutumika, sasa sisi kazi yetu ni kusimamia mpira tukiona upungufu huo tunaufungia tu ili wahusika wauweke sawa,” alisema Kasongo na kuwataka wamiliki na timu kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuwa na viwanja imara ili kuepusha fungia fungia.