Mke wa Victor Costa, Asha Baraka watoana jasho
Muktasari:
Katika Uchaguzi huo Mkuu wa Simba utakaofanyika Novemba 3, nafasi moja ya ujumbe ni lazima iwe ya mgombea mwanamke.
Wagombea wawili wanawake wanaowania ujumbe katika Bodi ya Klabu ya Simba, Asha Baraka na Jasmin Badar wamegeuka kivutio katika mdahalo wa wagombea wa klabu hiyo unaofanyika wilayani Temeke jioni hii.
Jasmin ambaye ni mke wa mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa na Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ASET inayomiliki bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' ni miongoni mwa wagombea 16 walioshiriki katika mdahalo huo.
"Nimeifanyia mengi Simba tangu nilipopata uanachama mwaka 1984 ikiwemo kuandaa tamasha ambalo fedha zote nilipeleka ndani ya klabu yetu. Naifahamu vyema Simba na nimeitumikia vya kutosha," alisema Asha Baraka.
Kwa upande wake, Jasmin alisema alama kubwa anayojivunia Simba ni timu yao ya wanawake.
"Mimi ndiye mwasisi wa timu yetu ya wanawake ya Simba Queens ambayo wakati tunaianzisha haikuwa na bajeti yoyote lakini kwa juhudi zangu nilipambana hadi ikaweza kusimama na sasa ni moja ya timu tishio na imara kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara," alisema Jasmin.