Miyeyusho kumbe naye yumo aisee

BONDIA Chichi Mawe au Francis Miyeyusho naye yumo kumbe! Mwanamasumbwi huyo mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam amemwangalia mpinzani wake, Loren Japhet akamchimba mkwara wa maana unaambiwa.
Si unakumbuka Miyeyusho atazichapa na Japhet Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Kines, Dar es Salaam? Siku ambayo pia mkali wa mwingine wa Masumbwi nchini, Mada Maugo atazichapa na Kanda Kabongo, Dulla Mbabe atazichapa na Benson Mwakyembe na Mfaume Mfaume atamaliza ubishi wake na Habibu Pengo.
Sasa buana Miyeyusho ambaye siyo mzungumzaji sana awamu hii kaamua kuvunja ukimya naye kaingia anga za Maugo na jana buana amemwambia Japhet eti kama asimpovunja taya basi atamtengua shingo kesho Ijumaa.
“Huyu ‘dogo’ anatafuta kifo tu, nikimwangalia hata raundi ya tatu hafiki, yaani nitampiga huku nalia kwa kumwonea huruma,” alisema Miyeyusho ambaye anaheshimika vikali katika mitaa ya Kinondoni Mkwajuni anakoishi.
Alisema maandalizi aliyoyafanya kwa ajili ya pambano hilo siyo ya kumkawiza Japhet na kama atacheza sana basi ataishia raundi ya tatu.
Mabondia hao ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitambiana wakati wakisubiria kukutana kwa mara nyingine tena, watapima uzito leo Alhamisi zoezi litakaloanza saa 3:30 Asubuhi kwenye Uwanja wa Kinesi, Shekilango.