Miujiza pekee kuiokoa Mtibwa

Muktasari:

  • Ina pointi 17 imesaliwa na mechi nane dhidi ya JKT Tanzania, Ihefu, Simba, Yanga, Azam, Mashujaa, Tabora Utd na Namungo ndio timu iliyoshinda mechi chache, ikishinda nne na imefungwa mabao mengi kuliko timu yoyote.

KUNA namna mbili ambazo zinaweza kuiokoa Mtibwa isishuke daraja ambazo ni kumaliza ikiwa juu ya nafasi ya 13 ambapo itabaki moja kwa moja ama kumaliza juu ya nafasi ya 15 ili iweze kupambana kubaki kupitia mechi za mchujo (play-off).

Ina pointi 17 imesaliwa na mechi nane dhidi ya JKT Tanzania, Ihefu, Simba, Yanga, Azam, Mashujaa, Tabora Utd na Namungo ndio timu iliyoshinda mechi chache, ikishinda nne na imefungwa mabao mengi kuliko timu yoyote.

Imezidiwa kwa tofauti ya pointi saba na timu iliyo katika nafasi ya 12 hivyo ili ikae hapo inapaswa kushinda mechi tatu na kuombea timu iliyopo katika nafasi hiyo ipoteze mechi tatu.

Lakini imezidiwa pia kwa pointi sita na Tabora United ambayo ipo katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23.

Kama inazidiwa kwa pengo kubwa la pointi na timu ambazo iko nazo chini, kuna kazi kubwa ambayo Mtibwa inapaswa kufanya ili ibakie Ligi Kuu msimu ujao vinginevyo itakuwa kwaheri ya kuonana.

Mtibwa Sugar inayoonekana kushindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Manungu Complex kupata matokeo mazuri imebakiza mechi nne nyumbani na nne ugenini.

Hadi sasa timu hiyo imecheza mechi tisa kwenye uwanja huo wa nyumbani na imepata ushindi mara mbili tu, kutoka sare mbili na kupoteza mechi tano, huku ikifunga mabao 11 na kufungwa 13.

Kwa sasa imebakiza mechi nne tu za nyumbani ambazo zitakuwa dhidi ya Azam FC, Tabora United, Yanga na Namungo FC, mechi nne za ugenini wataanza dhidi ya Simba, JKT Tanzania, Mashujaa na Ihefu.

Kimahesabu ikitokea Mtibwa, ikishinda mechi nne mfululizo itakuwa na pointi 29 zitakazoipa unafuu huenda ikaangukia kucheza mchujo kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita ambapo ilicheza dhidi ya Prisons na kusalia hata hivyo maafande hao na walijinasua.

Ukiachana na Ligi Kuu inayoendelea (2023/24), ndani ya misimu mitatu nyuma Mtibwa haikuwa kwenye kiwango cha ushindani na iliponea chupuchupu kushuka daraja.

Katika jumla ya mechi 30 ilishinda mechi tisa, sare nane na ilifungwa 13, ilimaliza msimu nafasi ya 10, ikiwa na pointi 35, zilizoifanya ikacheze play-off dhidi ya Mbeya City na kutoboa ikiiachia msala City iliyoenda kukutana na Mashujaa na kushushwa daraja kuzifuata Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zilizoteremka moja kwa moja.