Mirambo: Tumetanguliza mguu mmoja Kombe la Dunia

Muktasari:
Washindi wawili kutoka katika kila kundi pamoja na kutinga nusu-fainali pia wanakuwa wamefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia la U17, Oktoba nchini Brazil.
Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo, amesema kikosi hicho kimetanguliza mguu mmoja kucheza Kombe la Dunia na hatua waliyofikia hawawezi kurudi nyuma.
Timu hiyo inatakiwa kushinda michezo miwili au yote mitatu kwenye kundi lao katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON U 17) ili kujihakikishia kucheza Kombe la Dunia kwa vijana.
"Historia lazima iandikwe, kushiriki AFCON ni kama tumetanguliza mguu mmoja katika Kombe la Dunia na mguu wa pili tutamalizia kwenye mechi zetu za makundi," alisema kocha huyo.
Alisema watoto wake kama alivyozoea kuwaita, akili yao ni kucheza Kombe la Dunia. Kila mmoja ana ndoto ya kuweka historia hivyo hivyo ndoto lazima itimie.
Akizungumzia maandalizi ya timu yake kuelekea mashindano hayo, alisema wapo hatua ya mwisho.
"Washambuliaji sina tatizo nao, ninachokifanya sasa ni kuimarisha safu ya ulinzi ili nao wasifungwe magoli," alisema.
Serengeti Boys ipo kundi moja na Nigeria, Angola na Uganda kwenye fainali za Afcon 2019 zitakazoanza Aprili 14 jijini Dar es Salaam zikihusisha timu nane zili katika makundi mawili. Washindi wawili kutoka katika kila kundi pamoja na kutinga nusu-fainali pia wanakuwa wamefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia la U17, Oktoba nchini Brazil.