MIRAJI: Gari sasa limewaka

Muktasari:

WINGA matata wa Simba, Miraj Athuman ‘Sheva’ kwa sasa yupo kwenye mazoezi makali ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Dar es Salaam kuongeza kasi ya upachikaji mabao aliyoianza mwanzoni mwa msimu huu. Katika michezo mitano ya awali ya Ligi Kuu Bara tayari alikuwa amefunga mabao manne.

WINGA matata wa Simba, Miraj Athuman ‘Sheva’ kwa sasa yupo kwenye mazoezi makali ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Dar es Salaam kuongeza kasi ya upachikaji mabao aliyoianza mwanzoni mwa msimu huu. Katika michezo mitano ya awali ya Ligi Kuu Bara tayari alikuwa amefunga mabao manne.

Miraji mwenye mabao sita mpaka sasa kwenye Ligi Kuu mara ya mwisho kufunga ilikuwa Novemba 23 katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting wakati Simba ikishinda 3-0 huku akifunga mabao mawili na Tairone Santos akitupia moja kambani.

ANAJIFUA BALAA

Mwanaspoti lilibahatika kumnasa winga huyo akijifua kwenye Ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam pamoja na wachezaji kadhaa wa Ligi Kuu, ambapo alifunguka mengi juu yake.

“Kwanza nipende kumshukuru Mungu naendelea vizuri na mazoezi, nimepewa mazoezi maalumu na kocha ili kuona namna ambavyo nitaendana na yale wenzangu wanayofanya na walikuwa wakiyafanya nikiwa nje,” anasema Sheva.

“Kila kitu naamini kitakuwa sawa, nasubiri ligi irudi nione namna kocha atakavyoamua kama naweza nikaanza kurudi uwanja, lakini tayari nimepona ndio maana naendelea na mazoezi.

“Mazoezi ninayofanya ni yale ninayopewa na mwalimu kwa sababu kila mchezaji anapewa mazoezi yake ambayo unajisimamia mwenyewe.”

Anasema aina ya mazoezi anayofanya ni yale ya kumpa wepesi ndio aliyoambiwa ayafanye huku muda mwingi akionekana akikimbia.

HALI YA AFYA

“Kwa sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri tena sana ndio maana nafanya mazoezi ili niendelee kuwa fiti ila naendelea vizuri.

“Ligi ikirudi nina asilimia 90 ya kucheza, hizo nyingine inategemea na uamuzi wa mwalimu kwa namna ambavyo ataona.

“Kwa kweli nimemisi kucheza maana hiyo ndio kazi yangu na sijaonekana uwanjani muda mrefu, nadhani hilo litakuwa jambo jema nitakapoonekana kwa mara nyingine uwanjani,” anasema.

Anasema moja ya vitu ambavyo hataweza kuvisahau ni mwendelezo wa kufunga mabao katika michezo mfululizo aliyocheza mwanzoni mwa Ligi Kuu.

MALENGO YAKE

Miraji anasema moja ya malengo aliyoyaweka mwanzoni mwa msimu wakati akijiunga na timu hiyo ni kufikisha mabao 15, msimu huu.

Michezo aliyofunga msimu huu ni dhidi ya JKT Tanzania walioshinda 1-3 huku akifunga bao moja na Meddie Kagere mabao mawili.

Katika ushindi wa ushindi wa 2-1 mbele ya Mtibwa Sugar pia alitupia moja kama ilivyo kwa Kagere na walifunga tena wote wawili kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Biashara United.

Miraji aliipa Simba alama tatu kwenye ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha mbele ya Singida United kisha akatupia mabao mawili kwenye ushindi wa 3-0 mbele ya Ruvu Shooting.

HANA PRESHA

Wachezaji wengi wanaposajiliwa na timu nyingine huchukua muda mrefu hadi kuendana na mfumo wa timu anayocheza tofauti na Miraj alivyofanya baada ya kutua Simba.

“Kuna ushindani wa namba mkubwa ndani ya timu hiyo kutokana na kuwepo kwa wachezaji wazuri, hivyo unamfanya mchezaji kujituma na kuhakikisha anazidi kubaki kwenye ubora wake,” anasema mchezaji huyo.

“Kwa upande wangu nimewahi kucheza tangu nikiwa mdogo na kufanikiwa kupandishwa timu kubwa, hivyo sina ugeni mkubwa ndani ya timu hiyo ndio maana haijanisumbua sana.

“Kikubwa mashabiki waniombee ligi ikirudi tuweze kufanya vizuri tena na mambo mengine yazidi kuendelea kikubwa ni uzima.”

SVEN POA TU

Miraji aliyeaminiwa vyema na kocha Patrick Aussems aliyetimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sven Ludwig Vandenbroeck akisaidiana na Seleman Matola kwa sasa, anasema ni muda kila kitu kitanyooka. “Kocha bado hajapata nafasi ya kuniona tangu alipofika maana alinikuta nimeumia, naamini kipindi hiki nitakachopata nafasi ndio ataniona vizuri.

Anaongeza kuwa haoni tofauti kati ya Sven na Aussems maana wote kwake ni walimu na wanafanya kazi vizuri, hivyo hana wasiwasi juu yao.

Miraji amepitia klabu kadhaa kabla ya kurejea tena Simba ambako ndiko kipaji chake kilianzia na kuaminiwa. Miongoni mwa timu alizopita ni Toto Africans (2015-2016), Mwadui FC (2016-2018) na Lipuli FC (2018-2019).

Wakati akiwa Simba B alikuwa kwenye kile kizazi cha wachezaji wengi ambao waliitwa kama kizazi cha dhahabu cha Msimbazi.

Baadhi ya wachezaji waliotamba enzi hizo chini na Matola ni Jonas Mkude, Said Ndemla, Miraji Athuman, Haroun Chanongo, Edward Christopher, Omary Salim, Miraj Adam, Abdallah Seseme na Hassan Isihaka.