Mijengo ya mastaa hawa kufuru tupu

Muktasari:

  • Katika mahojiano maalumu baadhi ya wanariadha hao wamefunguka kuwa, wametokea kwenye familia duni na ilikuwa wakati wa mvua basi majumbani kwao ilikuwa hakuna kulala unaambiwa.

ARUSHA.KAMA supastaa wa Manchester United, Alexis Sanchez katoboa kimaisha na sasa analipwa mshahara mkubwa kuliko mastaa wa Ligi Kuu England, ni kwa nini wanariadha wa Kitanzania nao wasitoboe.

Kama hufahamu basi kuna mastaa kibao kwenye riadha ambao wametokea kwenye maisha duni, lakini kwa sasa wanakula bata kuliko vibosile kwenye taasisi za serikali na mashirika ya umma.

Ndio! Yaani kuna wanariadha licha ya kukosa fursa ya kusoma, lakini wanaishi maisha ya kibosi huku wasomi wakiyasikia tu.

Mwanaspoti limetia timu kwenye mijengo ya wanariadha wa timu ya taifa na kujionea mambo makubwa na mazito.

Katika mahojiano maalumu baadhi ya wanariadha hao wamefunguka kuwa, wametokea kwenye familia duni na ilikuwa wakati wa mvua basi majumbani kwao ilikuwa hakuna kulala unaambiwa.

Si kama walipenda iwe hivyo, lakini nyumba walizokuwa wakiishi hazikuweza kuwasitiri kipindi cha mvua, zilivuja na kusababisha maji kujaa ndani, lakini kwa sasa wamekichafua hapo Arachuga wakimiliki mijengo ya maana tu yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

Hebu wasikie wenyewe hapa.

FABIANO JOSEPH

Fabiano ni miongoni mwa wanariadha tegemeo wa timu ya taifa kwenye mbio ndefu (Marathoni na nusu marathoni au kilomita 42 na 21), nyota huyu mzaliwa wa Babati mkoani Manyara, ni mmoja wa wanariadha wenye mijengo ya maana tu pale Arusha.

Tena si mjengo mmoja, Fabiano ambaye ukimwangalia kwa haraka haraka unaweza kumdharau kutokana na umbile lake, lakini ana mijengo mitatu ya nguvu hapa Arusha.

Nyumba ambayo nyota huyu anaishi ni ya ghorofa moja ambayo mwenyewe anafichua imemgharimu Sh110 milioni hadi kukamilika, lakini anayo nyumba nyingine aliyoijenga kwa gharama ya Sh70 milioni hadi kukamilika na sasa ameshusha mjengo mwingine ambao, haujakamilika na ukikamilika basi Sh70 milioni nyingine itakuwa imelala hapa.

“Nyumba zote nimejenga kwa fedha ya riadha, hii ninayoishi (mjengo wa ghorofa) ni nyumba yangu ya pili iko Iliboru na imenigharimu Sh110 milioni,” anasema Fabiano bingwa wa zamani wa dunia wa nusu marathoni.

Nyumba ya kwanza kujenga ya mwanariadha huyo iko eneo linaitwa Visiwani ambayo anakwambia ametumia Sh70 milioni hadi kukamilika.

“Hiyo nyumba sasa nimewapangisha wazungu, nachukua kodi Dola 400 kwa mwezi, ni nyumba kubwa yenye vyumba vinne vya kulala, sebule mbili, jiko na master bed room, ina eneo la maegesho ya magari,” anasema Fabiano.

Mwanariadha huyo anajenga mjengo mwingine ambao haujakamilika pale Kwa Mrombo ambayo ina vyumba 24 na anakwambia hadi kukamilika anatarajia pia kutumia Sh70 milioni.

“Fedha ya kufanya yote hayo nimeipata kwenye riadha, asikwambie mtu riadha inalipa, sikusoma sana na sikuzaliwa katika familia tajiri, lakini riadha imebadili maisha yangu na ya wazazi wangu,” anasimulia Fabiano na kuendelea.

“Sikuwahi kufikiria kama kuna siku nitajenga nyumba ya maana, achilia mbali hii ya ghorofa ninayoishi, nyumbani kwetu tulikuwa na maisha magumu, nakumbuka kuna wakati nyumba yetu kijijini mvua ikinyesha kama ni usiku tumelala basi usingizi ndiyo basi tena, lazima tuamke,” anakumbuka mwanariadha huyo.

Kupitia riadha, Fabiano amewajengea pia wazazi wake nyumba ya maana tu kijijini kwao Gedamali.

GABRIEL GEAY

Mwanariadha huyu alianza kuvuma mwaka 2017 alipofuzu kushiriki mashindano ya dunia kule London, Uingereza.

Nyota huyo wa mbio ndefu za uwanjani (mita 5,000 na 10,000) nchini anajenga nyumba ya pili huko Ilboru, nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Geay anakwambia anatarajaia kutumia Sh60 milioni hadi mjengo huo kukamilika. Kwa sasa mjengo huo upo katika lenta.

Hiyo ni nyumba yake ya pili kuijenga kutokana na fedha za riadha, mjengo wa kwanza aliamua kuwajengea wazazi wake kijijini kwao Madunga, wilayani Babati.

FAILUNA ABDI MATANGA

Ukimwangalia Failuna kwa haraka haraka namna alivyo na mwili mdogo, unaweza kudhani labda anaishi nyumbani kwa wazazi wake. Lakini, binti huyo mwenye rekodi tamu ya riadha nchini ameamua kuwekeza kwenye mijengo.

Ukubwa wa nyumba ya Failuna kila mwanariadha anayemfahamu anauzungumiza, amenjenga nyumba ya maana tu iliyopo jirani na Sekondari Ilboru.

Ukiwa shuleni hapo, kuna barabarani yenye kilima ambayo kama si mtu wa mazoezi, kidogo utakusumbua kuupanda, ni mwendo kama wa dakika 10 kutembea katika kilima hicho ili kutokea upande wa pili iliko nyumba ya Failuna.

“Hii ni nyumba ambayo sitarajii kuishi hapa maisha yangu yote, nimeijenga kwa malengo ya kuja kuipangisha baadaye,” anasema Failuna, ambaye amejenga nyumba nne tofauti ndani ya eneo hilo.

Kila nyumba inajitegemea ingawa ziko ndani ya fensi moja, na alichokifanya Failuna ni kumalizia moja ambayo ina vyumba viwili na sebule ambako anaishi na nyingine tatu kila moja ikiwa na vyumba viwili na sebule, akiendelea taratibu.

“Natarajia kutumia kati ya Sh80 milioni hadi 90 kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi,” anasema Failuna.

Mwanariadha huyo anakwambia, fedha ya mjengo huo imepatikana kwenye mbio zake binafsi ambazo zimekuwa zikimwingizia mkwanja wa maana tu.

“Nitakapoikamilisha hii nyumba ya Ilboru, sitokaa hapa hapa muda mrefu nafikiria kujenga mjengo mwingine mbali na eneo hili na hii nyumba nitaipangisha ili iwe ikiniingizia kipato,” anasema Failuna.

ALPHONCE FELIX SIMBU

Bingwa huyu wa mbio za Standard Chartered za 2016 na mshindi wa medali ya shaba ya dunia ana mjengo wake wa nguvu tu eneo la Ngateu, ambao umepatikana kwa fedha ya riadha.

Simbu anakwambia ametumia Sh70 milioni kukamilisha mjengo huo ambao ndiko anaishi na familia yake yenye mtoto mmoja, Abednego.

“Yote ni sababu ya riadha, nauheshimu sana huu mchezo sababu bila riadha sijui maisha yangu yangekuwaje, lakini leo hii achilia mbali nyumba, lakini nimefanya mambo mengi tu ya maandeleo kwa fedha ya riadha,” anasema mwanariadha huyo na mshindi wa medali ya fedha ya dunia.

EMMANUEL GINIKI

Mwanariadha huyu nyota wa mbio ndefu za uwanjani na barabarani naye ana mjengo wake wa nguvu tu kijijini kwao pale Katesh.

Mjomba wa Giniki, Gidamis Shahanga aliyeko Katesh anasema kwa umri wa mwanariadha huyo na mjengo alioujenga kijijini ni kitu kikubwa.

“Amejenga nyumba nzuri sana kijijini, ambayo amejenga kama ya familia,” alisema Gidamis mwanariadha nyota wa zamani na bingwa mara mbili wa Jumuiya ya Madola.

Giniki mwenyewe anakwambia riadha imempa heshima, imemfanya awe mfano wa kuigwa na vijana wengine kijijini kutokana na mafanikio yake.

“Siwezi kusema nimetumia kiasi gani hadi kukamilisha nyumba hii, lakini yote nimeyafanya kwa fedha ya riadha,” alisema Giniki ambaye anakwambia siku si nyingi atashusha mjengo mwingine pale Arusha anapoishi kwa sasa.

Mbali na wanariadha hao, pia mkongwe wa mbio za kati, Filbert Bayi ana mjengo wake wa nguvu pale Kibaha Mkuza ambao, wakazi wa eneo hilo wameupachika jina la ‘White House’ kutokana na namna ulivyo bomba.

Wengi wa wanariadha wamebadili maisha yao kutokana na vipaji vya kufukuza upepo ambavyo hakuna gharama kufika huko zaidi ya juhudi na kujitolea kwa mchezaji kufanya mazoezi na kutaka mafanikio.