Miguu ya Banda yabadili maisha ya familia

Muktasari:
Mama yake amefunguka mambo mengi kuhusiana na Banda, kuanzia maisha yake tangu utotoni, kipaji chake kilivyoanza kuchomoza na mipango yake ya baadaye
Dar es Salaam. KWA sasa Zabibu, mke wa beki wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kwenye klabu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, yuko zake Tanga kwa mama mkwe wake, Mwanahawa Mwalimu. Nadhani utakuwa unajiuliza shavu linaloendelea kumtoka Zabibu na kumfanya kuzidi kunawiri, jibu ni moja tu ndoa yake ina furaha na inanogeshwa zaidi na mama mkwe wake huyo kutokana na kuishi kwa maelewano na furaha.
Asikwambie mtu ndoa ni tamu sana bana na hilo linadhihirika kwa Zabibu, ambaye ni mdogo wa staa wa Bongo Flava, AliKiba na AbduKiba.
Mfululizo wa makala haya ya mahojiano maalumu na Zabibu, ambaye ameeleza mambo mbalimbali kuhusu yeye na mumewe Banda, leo tutaangalia kwa upande wa Mwanahawa. Mama huyu amefunguka mambo mengi kuhusiana na Banda, kuanzia maisha yake tangu utotoni, kipaji chake kilivyoanza kuchomoza na mipango yake ya baadaye. Pia, unafahamu baba yake Banda alicheza soka kwenye klabu maarufu nchini? Unajua Banda shuleni alikuwa bonge la kichwa yaani akili mingi mingi sana? Endelea kutiririka…
“Namshukuru Mungu kwa Banda kwani, ni mpole na mwenye heshima na shuleni alikuwa na akili nyingi sana. Yanapokuja matokeo basi huwa nategemea namba moja, mbili ama tatu.
"Banda alikuwa ni mtu wa kujituma, alikuwa akitoka shule anafanya kazi zote za nyumbani ambazo alipewa kisha kuendelea na ratiba nyingine, ikiwemo kwenda madrasa na mazoezini.
"Alikuwa akimudu kivifanya vyote kwa usawa. Banda ni mpole tofauti na wengi wanavyomchukulia, pia sio mtu wa magenge," anaanza kwa kusema Mwanahawa.
MSOSI WAKE UTOTONI
Mzazi ndio Mungu wa pili hapa duniani na kwa Banda mtu anayemfahamu kwa undani kabisa ni mama yake, Mwanahawa. Kuna vitu vingi ambavyo Banda alikuwa akipenda tangu akiwa mtoto na kwenye sekta ya misosi ndio usisema kuna ile ambayo ilikuwa ikimpa mzuka kinoma.
"Tangu akiwa mtoto alikuwa anapenda sana maharage, mbaazi na anakula na chapati, lakini mihogo ya nazi kwake analia na samaki.
"Hicho ndo chakula ambacho hata kama akitoka Afrika Kusini huwa najiandaa kumuandalia kwa sababu ni chakula kinachomrudisha utotoni," anasema.
KIPAJI CHAKE
Mama wa Banda, anasema mwanzoni hakuwa akimsapoti sana mwanaye, lakini alivyoona anaweza kurithi mikoba ya baba yake akaamua kumuunga mkono.
"Banda amerithi kipaji kutoka kwa baba yake, nilikuwa nikipiga sana vita kucheza soka lakini baadaye niligundua kuwa, nakosea maana kama ni kucheza kwake soka mwanzilishi ni baba yake," anasema.
“Baba yake na Banda ambaye alitamba Simba kwenye miaka ya 90, alikuwa akicheza kama kiungo mkabaji licha ya kuwa na uwezo pia wa kucheza nafasi nyingine.
“Mtoto naye ana uwezo kama wa baba yake wa kucheza zaidi ya nafasi moja, Banda anamudu kucheza kama kiungo mkabaji, beki wa kati na muda mwingine anaweza kucheza beki ya kushoto, anaongeza Mwanahawa.
Lakini, kama ilivyokuwa kwa baba yake, Banda naye kabla ya kutua Simba alikuwa akiichezea Coastal Union ya Tanga, kisha akasepa zake Afrika Kusini.
AJIVUNIA BANDA
Mama Banda anaweka wazi kuwa pamoja na mwanzo kujaribu kupinga kipaji cha mwanaye, lakini sasa anafurahia matunda yake kwani maisha yamekuwa na maana kubwa.
"Sikuwahi kufikiria kama Banda ataweza kunijengea nyumba kupitia kazi yake ya soka kama alivyofanya, nguvu kubwa nilielekeza katika elimu yake ambayo hata hivyo, hakuweka kufika mbali kutokana na kujikita katika soka.
"Nyumba aliyonijengea iliyopo eneo la Duga imetokana na usajili wake kwenda Simba ambao, umefanikisha kuinua nyumba hiyo ambayo imekamilika japo sijahamia ikisubiri vitu vidogo tu," anasema.
Mbali na mjengo huo, Banda pia yupo katika hatua nzuri za ujenzi wa mjengo wake wa maana uliopo Mwambani, ambalo ni eneo la kishua kama ilivyo Masaki, Dar es Salaam.
BANDA AMVUTIA KASI DROGBA
Nyota wa Baroka FC, Abdi Banda kumbe ana ndoto za kufanya biashara baada ya kustaafu soka kama ilivyo kwa Didier Drogba.
Mama yake amesema kuwa staa huyo wa zamani wa Simba ana akili ya biashara tangu akiwa mdogo.
"Huwa nakaa chini na mwanangu ili kujua mipango yake ya baadaye kwa sababu soka linachezwa kwa kipindi Fulani tu, mar azote anasema biashara ndio kila kitu kwake.
"Tayari kuna vitega uchumi anavyo ila siwezi kusema kwa kuwa ni maandalizi ya maisha yake baada ya soka, sitegemei kumwona anaangaika baada ya kustaafu," anasema Mwanahawa.
AMKUBALI KICHUYA
Mama Banda hakutaka kuficha hisia zake kwa winga wa Simba, Shiza Kichuya namna ambavyo anakubali akiwa uwanjani. Pia ni shabiki wa Simba na alianza kujipenda kabla ya Banda kujiunga nayo akitokea Coastal.
"Kwa sasa sio shabiki sana, lakini wakati Coastal ikicheza na Simba na Banda akiwa uwanjani. Niliumia sana kwani siku hiyo aliumia na sikwenda tena.
HUMWAMBII KITU KWA ZABIBU
Mama Banda ameweka wazi namna ambavyo anamchukulia mkwe wake, Zabibu kuwa ni mtoto wake wa kumzaa na kueleza kwamba, wako huru kuzungumza lolote.
"Zabibu ni mwanangu sio mkwe naishi naye vizuri kama binti yangu na nikikaa naye hapa Banda anajisikia amani zaidi kuliko akiwa Dar," anasema.