Migne achekelea Wanyama kurejea

Muktasari:

Harambe Stars inayoshika nafasi ya pili katika kundi F, ikiwa na pointi tano sambamba na vinara wa kundi, Ghana lakini ikizidiwa kwa tofauti wa mabao, inahitaji kushinda mchezo wa Jumatano kuweka sawa kampeni yao ya kusaka tiketi ya kuelekea Cameroon mwakani.

Nairobi, Kenya. Kundi la pili la timu ya taifa, Harambee Stars, linatarajiwa kuondoka leo jioni kuelekea Ethiopia kwa ajili ya mechi ya kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika, huku Kocha mkuu Sebastien Migne, akifurahia uwepo wa Nahodha wake, Victor Mugubi anayekipiga katia klabu ya Tottenham Hotspurs ya England.

Hakikisho la kurejea kwa Wanyama, limekuja wakati ambao Stars ambayo ipo kundi F, Sambamba na Ghana, linahitaji huduma za kiungo huyo mkabaji zaidi kuelekea mtanange huo mgumu utakaopigwa katika dimba la Bahir Dar, siku ya Jumatano, Oktoba 10.

Akizungumza na waaandishi wa habari jana, katika uwanja wa kimataifa wa Ndege wa Kenyatta, kabla ya kukwea pipa na kundi la kwanza la Stars, Migne ambaye alishindwa kuzuia furaha, alisema wa Wanyama utakiongezea kikosi chake morali katika mechi hiyo ambayo Stars inahitaji ushindi kujiweka sawa katika kampeni yake.

Wanyama alikosa mechi ya pili ya kundi F, dhidi ya Ghana iliyopigwa ugani Kasarani na Stars ikashinda 1-0, kutokana na kutokuwa katika hali ya utayari wa kuingia uwanjani, kwa sababu alihitaji muda wa kujiweka sawa baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yamemuweka nje ya uwanja kwa muda.

 

“Tulishinda mchezo dhidi ya Ghana bila nahodha wetu. Kurejea kwake kikosini kutasaidia kupandisha morali na matumaini yetu kuwa Jumatano tunakwenda Bahir Dar, kupata ushindi kabla ya kurejea nyumbani kufunga kazi. Nimefarijika sana kusikia yuko tayari na ataungana nasi siku ya Jumatatu,” alisema Migne.

Baada ya kundi la kwanza lililojumuisha nyota watano ambao ni mlinda mlango wa Bandari, Farouk Shikhalo, Abdallah Hassan (Bandari), Philemon Otieno na Francis Kahata kutoka Gor Mahia pamoja na Straika wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga, kundi la pili linatarajia kuondoka kesho sambamba na nyota wa kimataifa.

Mbali na watano hao, kundi la pili litakaloondoka kesho litajumuisha nyota wanne wanaosakata soka humu nchini, ambao ni Pitson Mutamba, Patrick Matasi, Dennis Odhiambo  na Bernard Ochieng. Wanne hawa wataungana na akina wanyama na wenzake.

Kikosi kamili kitakachoondoka kesho ni Piston Mutamba (Sofapaka), Patrick Matasi (Tusker, Kenya), Dennis Odhiambo (Sofapaka, Kenya), Benard Ochieng (Vihiga United, Kenya), Musa Mohammed (Nkana FC, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg FC, South Africa), Abud Omar (Cercle Brugge, Belgium), na David Ochieng (IF Brommapojkarna, Sweden).

Wengine ni, Erick Ouma (Vasalund, Sweden), Ismael Gonzales (Las Palmas, Spain), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, England), Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Belgium), Paul Were (FC Kaisar, Kazakhstan), Michael Olunga (Kashiwa Reysol), Erick Johanna (IF Brommapojkarna), Ovella Ochieng (Vasalund).