Mibuyu hii sasa inang’oka Msimbazi

Muktasari:

  • Hali hiyo inatokea wakati Simba ikikabiliwa na kibarua cha kushinda mechi nane za ligi kuanzia ile ya Ijumaa iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar ili kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwezekana kutoa ushindani katika ubingwa huku ikiiombea matokeo mabaya Azam iliyoshika nafasi ya pili na vinara Yanga.

WAKATI Simba ikiendelea kupiga hesabu za kumaliza msimu na kuanza usajili mkubwa ikiwemo kumshusha kocha mkuu mpya baada ya Abdelhack Benchikha kuondoka, kuna mibuyu itang’oka punde na mingine itajivunja.

Hali hiyo inatokea wakati Simba ikikabiliwa na kibarua cha kushinda mechi nane za ligi kuanzia ile ya Ijumaa iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar ili kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwezekana kutoa ushindani katika ubingwa huku ikiiombea matokeo mabaya Azam iliyoshika nafasi ya pili na vinara Yanga.

Simba ikishinda mechi zake itafikisha alama 71 ambazo Azam itazivuka kama ikishinda mechi zake zote zilizobaki itafikisha 72. Ikumbukwe timu hizo zina mechi moja ambayo zitakutana zenyewe.

Wakati Simba ikipiga hesabu hizo kuelekea kuhitimisha msimu huenda itawakosa wachezaji wake muhimu kwa nyakati tofauti kutokana na sababu mbalimbali kama zinavyoainishwa hapa chini ambazo huenda zikawa pigo kwa timu;


CLATOUS CHAMA

Simba itapata pigo lingine kwa kumkosa Chama katika michezo kadhaa baada ya kiungo huyo kufungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu kutokana na kosa la kumkanyaga kwa makusudi beki wa Yanga, Nickson Kibabage wakati wa mchezo uliozikutanisha timu hizo huku Yanga ikishinda 2-1.

Hata hivyo, huenda mashabiki wa Simba wasimuone tena Chama uwanjani msimu huu kwani tayari ametimkia nchini kwao Zambia kutokana na kuwa majeruhi ikielezwa amekwenda kutibiwa.

Ukiachana na kutocheza mechi zilizobaki msimu huu, pia huenda ikawa mwisho wa Chama ndani ya Simba kwani mkataba wake unatamatika mwisho wa msimu huu na inaelezwa mazungumzo ya kumwongezea mkataba mpya hayajaeleweka huku kiungo huyo akihusishwa kuhitajika na Yanga.

Chama msimu huu ameifungia Simba mabao saba kwenye ligi na kutoa pasi za mwisho sita.


AYOUB LAKRED

Jambo lingine ambalo linaitikisa Simba kwa sasa ni kuhusu hatima ya kipa wake namba moja Mmorocco, Ayoub Lakred.

Mwanaspoti limejuzwa kipa huyo hana mpango wa kusalia Simba baada ya msimu huu kumalizika kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwake.

Simba inapambana kumwongezea mkataba kipa huyo lakini bado mazungumzo yanagonga mwamba na inaelezwa Ayoub anataka kuondoka baada ya kocha Benchikha na wasaidizi wake kuondoka hivyo hana msimamizi mzuri ndani ya timu hiyo.

Jambo hili ni pigo kwa Simba kwani Ayoub alikuwa ameanza kufanya vizuri na kuziba vyema pengo la Aishi Manula mwenye majeraha ya muda mrefu.

Kutokana na hilo Simba kimya kimya imeanza kusaka kipa mwingine.


KIBU DENIS

Jambo lingine lililowakalia vibaya viongozi wa Simba ni juu ya mkataba wa winga Kibu Denis kutamatika mwisho wa msimu huu.

Ndani ya Simba kuna mvutano na baadhi ya viongozi wanataka staa huyo aliyetua Simba misimu miwili iliyopita akitokea Mbeya City abaki lakini wengine wanataka aondoke.

Hata hivyo Kibu mkononi mwake ana ofa za timu mbalimbali Afrika zinazomhitaji lakini ametoa kipaumbele kwa Simba ambayo inaelezwa anahitaji zaidi ya Sh300 milioni ili kusaini mkataba mpya.


HENOCK INONGA

Baada ya kutua Simba misimu miwili iliyopita na kuimarisha eneo la ulinzi la timu hiyo, beki huyu anayesifika kwa kuzuia na kucheza kwa akili anatarajiwa kuondoka Msimbazi baada ya msimu huu kumalizika.

Inonga anatajwa kuhitajika zaidi na FAR Rabat ya Morocco anayoinoa kocha wa zamani wa Yanga, Nassredine Nabi na inaelezwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea.

Inaelezwa beki huyo hana furaha tena ndani ya Simba na hayupo tayari kuongeza mkataba mpya baada ya huu wa sasa kutamatika mwisho wa msimu.

Hili ni pigo lingine kwa Simba kwani kama Inonga ataondoka basi timu hiyo italazimika kutafuta mbadala wake.


SAIDI NTIBAZONKIZA ‘SAIDO’

Huyu ni kiungo mshambuliaji wa Simba anayeongoza kwa mabao kikosini hapo kwa wachezaji waliopo sasa akiwa nayo saba sawa na Mzambia, Clatous Chama.

Saido mwenye asisti mbili hadi sasa, Mwanaspoti linajua huenda kiungo huyo kutoka Burundi akakosa baadhi ya mechi nyingi muhimu za Simba zilizosalia jambo ambalo litakuwa pigo kubwa kwa timu hiyo uwanjani.

Sambamba na hilo, baada ya msimu huu kuisha inaelezwa kwamba ataondoka kwani mkataba wake unaisha na hakuna mpango wa kuongeza.

Mwanaspoti linajua Simba tayari imepanga kumpiga chini Mrundi huyo ili isajili mchezaji mwingine atakayeipa Simba mafanikio zaidi ingawa hata kwenye mitandao mashabiki wamekuwa na mitazamo tofauti.

Umri mkubwa ni miongoni mwa sababu zinazomuondoa Saido ndani ya Simba baada ya kudumu kikosini hapo tangu alipotua kwenye dirisha dogo la usajili la msimu uliopita na kuibuka mfungaji bora msimu huo akifunga mabao 17 na kutoa asisiti 12.


MAKOCHA, MASTAA WAFUNGUKA

Kocha mkongwe Sunday Kayuni, alisema kinachozisumbua timu nyingi hazina falsafa ili kocha akija aingie kwenye mifumo ya wachezaji, hivyo anapopewa timu anakutana na wale ambao hawaendani na falsafa yake.

“Ulaya timu zina falsafa zake, hivyo  zinakuwa zinaajiri maskauti wanaotafuta wachezaji wanaoendana na falsafa za klabu, hata wakitafuta kocha anakuwa wa aina hiyo, ndio maana inafikirisha kuona Simba itapata pigo gani kuwakosa wachezaji hao.

“Itategemea na mbadala wa wachezaji watakaowasajili, kocha watakayemleta je ataendana na falsafa ya wachezaji ambao atawakuta ama wamlete kocha ambaye atapewa nguvu ya kusajili wachezaji ambao wataendana na mifumo yake, kiukweli siwezi kuzungumza nje ya jicho la ufundi,” alisema Kayuni ambaye mwaka 1998 aliipa ubingwa AFC Leopards ya Kenya akiwa kocha mkuu.

Aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’, alisema akiondoka kipa Ayoub anaona mbadala wake anaweza akawa kipa wa Tabora United, John Noble Barinyima na yule wa Coastal Union, Ley Matampi.

“Shida haipo kwa wachezaji hao wakiondoka, ila ipo kwa skauti kujaza wachezaji wa kigeni wasio na hadhi ya timu, wanapaswa kusajili wageni wachache ghali na wenye uwezo wa kuisaidia timu kunyakua mataji ya nje na ndani,” alisema na kuongeza;

“Kama Fiston Mayele aliondoka Yanga na bado timu yao imesimama sasa shida ya Simba ni ipi, hapo lazima wajihoji, binafsi naamini  MO Dewji (Mohamed) ana uwezo wa kusajili wachezaji wazuri, ambao wanaweza wakabeba taji la Afrika na kama ameshindwa basi ashuke kwa wanachama.”