Miaka 9, Mwakinyo, wenzake washindwa kumng'oa Matumla kileleni

Licha ya kustaafu masumbwi tangu 2013, Rashid Matumla ameendelea kuwa bondia bora wa muda wote akiwafunika mabondia wote nchi kwenye viwango vya ubora.

Bondia huyo bingwa wa zamani wa dunia wa WBU ametajwa kuwa bondia bora wa muda wote kwa miaka tisa mfululizo tangu alipotundika glovu.

Mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) umemtaja Matumla au Snake Man kama anavyopenda kujiita kuwa ndiye bondia bora wa muda wote wa Tanzania, huku wakongwe wengine saba wakiingia kwenye 10 bora.

Kizazi cha sasa ni mabondia watatu pekee wameingia kwenye 10 bora wakiongozwa na Hassan Mwakinyo ambaye amekamata nafasi ya tatu akiwa na pointi 14.32 alizovuna tangu 2015 alipoingia kwenye ndondi akiachwa kwa pointi tano na Matumla ambaye ana 19.13.

Rogers Mtagwa anayeishi Marekani ametajwa kwenye nafasi ya pili akiwa na pointi    17.52 ambazo hazijafikiwa na bondia yoyote tangu 2014 alipostaafu masumbwi.

Joseph Marwa ambaye alistafu sanjari na Matumla, ametajwa kwenye nafasi ya nne akiwa na pointi 13.27 akifuatiwa na Ibrahim Class Mgender ambaye Julai atapanda ulingoni jijini Dar es Salaam.

Bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka    ambaye tangu 2018 hajapanda ulingoni amekamata nafasi ya sita akiwa na pointi 7.390 akifuatiwa na Francis Miyeyusho mwenye pointi 7.012.

Mbwana Matumla aliyetudika glovu tangu 2017 amekamata nafasi ya nane akiwa na pointi 6.781 huku Mambea Bakari liyestaafu ndondi miaka 20 iliyopita akitajwa kwenye nafasi ya tisa akiwa na pointi 6.759 na Anthony Mathias akihitimisha 10 bora akiwa na pointi 6.367.