Miaka 12 ya Adi Yussuf kucheza soka England

Tuesday June 22 2021
yusuph pic
By Eliya Solomon

MTANZANIA Adi Yussuf ambaye mkataba wake umemalizika wa kuichezea Blackpool ya daraja la kwanza ‘Champioship’ , ametimiza miaka 12 ya kucheza soka la ushindani nchini England, ni zaidi ya miaka mitatu ukimlinganisha na Lijendari wa Chelsea na timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba.

Dunia inamtambua Drogba kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari wa kiafrika kutokea kutokana na yale ambayo aliyafanya akiwa na Chelsea, bila shaka mtakuwa mnamkumbuka vile alivyokuwa akiwapapatua mabeki wazembe na kuwatungua makipa mbalimbali kwenye EPL, Kombe la FA, Carabao, Europa Ligi na hata Ligi ya Mabingwa Ulaya tofauti na Adi ambaye miaka hiyo ameitimiza akiwa anacheza nchini humo katika Ligi za madaraja ya chini.

Licha ya kwamba Adi mwenye umri wa miaka 29, alilelewa kwenye akademi ya Leicester City hakuwahi kupata nafasi ya kupenya hadi kikosi cha kwanza cha timu hiyo, zaidi alitolewa kwa mkopo Tamworth, 2011 kabla ya mkataba wake kumalizika kisha kujiunga na Burton Albion.

Adi ameonyesha kwamba haikuwa jambo jepesi kwake kutimiza miaka 12 ya kucheza soka la ushindani nchini humo kwa kusema, “Alhamdulilah msimu mwingine tena umemalizika, ni jambo jema kutazama nyuma na kujivunia kwa kutimiza mwaka wangu wa 12 kama mchezaji wa kulipwa,” alimalizia kwa usemi aupendao kuwa bila bao hawezi kupata usingizi.

Makala hii inakujia kwa mfumo wa takwimu wa namba kama ambavyo watoto wa mjini wamekuwa wakipenda kusema, zitaonyesha yale ambayo amefanya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania ambaye alizaliwa visiwani, Zanzibar, Februari 20,1992.

Advertisement