Mhilu awatoa hofu mashabiki Geita Gold

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, winga huyo wa zamani wa Kagera Sugar, alifunguka mipango madhubuti na masilahi mazuri yamembakisha Geita Gold na kuamua kuungana na viongozi wa timu hiyo wanaopambana kuirejesha Ligi Kuu.
WINGA wa zamani wa Yanga na Simba, Yusuph Mhilu msimu ujao atacheza Ligi ya Championship akiwa na kikosi cha Geita Gold baada ya kuongeza mkataba wa mwaka mmoja, huku akitaja sababu zilizomfanya aamue kubakia kwenye timu hiyo iliyoshuka daraja.
Mhilu ambaye alimaliza mkataba na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu, mwishoni mwa wiki iliyopita klabu hiyo imetangaza kumwongezea mkataba mwingine akiwa ni usajili wao wa kwanza baada ya mastaa wengi kutimka na kusaka malisho Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, winga huyo wa zamani wa Kagera Sugar, alifunguka mipango madhubuti na masilahi mazuri yamembakisha Geita Gold na kuamua kuungana na viongozi wa timu hiyo wanaopambana kuirejesha Ligi Kuu.
“Watu walitegemea niwe Ligi Kuu, wanadhani daraja la kwanza umeshuka kiwango, lakini mpira wa sasa hauko hivyo, soka limekua, kwa hiyo kama mchezaji unashawishika na malengo na masilahi yanayowekwa na timu husika,” alisema Mhilu na kuongeza;
“Viongozi wamenishawishi kwa malengo yao nikaona yanaendana na ya kwangu nikakubali nibaki tupandishe timu kwa sababu huwezi kulikimbia tatizo, nimeona nianze upya na Geita Gold tuirudishe Ligi Kuu.”
Akitoa ahadi kwa mashabiki wa timu hiyo, aliwatoa hofu na kuwataka wamwamini kwani soka ni mchezo wa wazi na ameamua kucheza Championship lakini ana imani atarudi kwenye kiwango chake na kurejea tena Ligi Kuu.
“Mashabiki wa Geita Gold waendelee kuiamini timu yao na waamini timu msimu ujao itapanda Ligi Kuu kwa sababu tumeona juhudi za viongozi, wanafanya kila kitu kuhakikisha wanaipandisha tena,” alisema Mhilu.