Mhilu ajishtukia, aingia chimbo

Muktasari:

  • Mhilu alisema kipindi hiki ambacho ligi imesimama anaendelea na mazoezi binafsi na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili asishuke kiwango chake na kujihakikishia namba.

BAADA ya kuanza kuaminiwa na benchi la ufundi winga wa Geita Gold, Yusuph Mhilu amesema anahitaji kuendeleza ubora wake akiahidi kutumia vyema mapumziko ili kubaki kikosi cha kwanza.

Nyota huyo hakuanza vyema msimu kutokana na maumivu ya goti yaliyomuweka nje kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kurejea Desemba 16, mwaka.

Tangu arejee uwanjani, staa huyo wa zamani wa Simba, Yanga na Kagera Sugar amekuwa na uhakika wa namba chini ya kocha mkuu, Denis Kitambi akicheza mechi 10 na kufunga mabao mawili.

Mhilu alisema kipindi hiki ambacho ligi imesimama anaendelea na mazoezi binafsi na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili asishuke kiwango chake na kujihakikishia namba.

Alisema baada ya kuaminiwa na kocha, anahitaji kuendeleza ubora wake ili kutopoteza namba kwenye kikosi cha kuanza kila mechi akieleza kuwa bado makali yake hayajatimia kama alivyokuwa awali.

“Binafsi natumia mapumziko haya kujituma zaidi na mazoezi binafsi na yale ya kocha na kurekebisha makosa madogo ninayoyafanya uwanjani na kujifunza mbinu mpya.”

“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri na matokeo ya mechi zetu za mwisho tulifanya vizuri kwahiyo haya mapumziko yatatuongezea kitu cha ziada,” alisema nyota huyo.