Mgunda atema madini, mastaa wafungiwa darasani

JUMAMOSI, kikosi cha Simba kitaondoka kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Agosto kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye.

Benchi la Ufundi la Simba chini ya kocha, Juma Mgunda katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo walitumia dakika si chini ya 45 kuwapiga darasa wachezaji wake kwenye mambo ya msingi.

Kwenye darasa hilo Mgunda akiwa na wasaidizi wake wawili, Selemani Matola na Mtaalamu wa uchambuzi wa mechi kupitia video, Culvin Mavunga waliweka mechi mbalimbali za Agosto na kuwaacha wachezaji wao waangalie ili kila mmoja kufahamu wapinzani walivyo haswa wakiwa nyumbani kwao.

Baada ya kuangalia mechi hizo, Mgunda na wenzake waliwalekeza wachezaji wao vile ambavyo Agosto wanashambulia, namna wanavyokaba wakiwa hawana mpira pamoja na aina yao ya kuutafuta mpira.

Mgunda aliwaonyesha wachezaji wake ubora wa wapinzani wao wakiwa na mpira na jinsi ambavyo wanashambulia yakiwemo madhaifu yao pindi wakati hawana mpira na namna ya kuyatumia ili kupata matokeo mazuri.

Hakuishia hapo, aliwaonyesha wachezaji wake vile ambavyo Agosto wanacheza wakiwa uwanja wa nyumbani kwenye mechi za mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ni muhimu zaidi kwa Simba safari hii.

Vile vile, namna gani wanatakiwa kuwazuia wachezaji wao hatari pamoja na mpango wa wapinzani wao ambao watakutana nao ugenini ili kufanikiwa kupata matokeo mazuri na kusonga mbele kwani wamepania breki ya kwanza iwe nusufainali.

Baada ya kupitia video hizo, Mgunda alisema; “Baada ya kuyaona yote hayo tumekwenda uwanja wa mazoezi kuyafanyia kazi kulingana na wapinzani walivyo nina imani tutapata matokeo mazuri ugenini na kuja kumaliza kazi mchezo wa marudiano nyumbani.”

“Ushindi dhidi ya Dodoma Jiji umeongeza hali na morali ya ushindani kwa wachezaji wetu ninaamini watakwenda kupambana na kupata matokeo bora ugenini ,Kuhusu Hennock Inonga maendeleo yake ni mazuri na yupo chini ya uangalizi wa madaktari ili kupata matibabu zaidi kutokana na shida aliyoipata na naamini tutakwenda nae Angola.”

Simba tayari imeshatanguliza mashushushu nchini Angola ili kuweka mambo sawa. Lakini juzi wakati nyota wa Simba wakitoka vyumbani kwenda kupasha kabla ya mechi kuanza akiwa kikosi cha kwanza, alishindwa na kutolewa baada ya kujisikia vibaya hivyo kuondolewa kikosini ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Kennedy Juma.