Mgunda apeta, Djuma atetea mastaa wake

SIMBA imepata ushindi wa mabao 3-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliyopigwa leo Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Dodoma Jiji.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na beki wa kati wa Dodoma Jiji, Abdallah Shaibu aliyejifunga dakika ya 6, Moses Phiri yote kipindi cha kwanza.

Bao la tatu lilifungwa na Habibu Kyombo kwa mpira wa kichwa dakika chache baada ya kuchukua nafasi kwa nahodha, John Bocco.

Baada ya ushindi huo Simba inapanda hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 13 katika michezo mitano iliyocheza hadi sasa.

Dodoma Jiji baada ya kupoteza imekwenda hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi sita na kufikisha pointi tano.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda amesema ushindi huo umetokana na wachezaji wake kufuata yale maelekezo ambayo aliwapatia katika mazoezi.

“Dodoma haijaanza Ligi vizuri msimu huu lakini ni miongoni kwa timu bora tumewafanyia kazi baada ya kuwaangalia hadi kufanikiwa kupata ushindi huu mkubwa,” amesema Mgunda na kuongeza;

“Ushindi huu umeongeza hali na morali kwa wachezaji wangu kuelekea katika mchezo wa kimataifa ambao ndio unafuata naimani napo huku tutafanya vizuri.”

Kocha wa Dodoma Jiji, Masoud Djuma amesema wachezaji wake walikuwa na mchoko kutokana na muda mchache uliokuwa nao tangu kucheza mechi ya mwisho huku wakisafiriw.

“Kipindi cha pili wachezaji wangu walichangamka tofauti na ilivyokuwa mwanzo wa mchezo na hapo tuliwapa ushindani wa kutosha Simba,” amesema Djuma aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba na kuongeza;

“Mchezo huo umekwisha sasa wanakwenda kufanya maandalizi na kurekebisha makosa yao kabla ya kucheza na Ihefu ili kupata matokeo mazuri tofauti na hayo dhidi ya Simba.”