Mgosi aichokoza Yanga

Muktasari:
Mchezo huo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la FA, unatarajia kuchezwa Jumapili, ambapo mshindi atakutana na Namungo ili kucheza nae hatua ya Fainali.
KOCHA mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema kuwa, kwa kiwango ambacho kimeoneshwa na timu yake ni kikubwa chenye uwezo wa kucheza na timu ya wanaume ya Yanga, kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.
Simba Queens jana Ijumaa ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake dhidi ya Yanga Princess na kuibuka na ushindi wa bao 5-1, mechi iliyochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, matokeo ambayo yamempa kiburi Mgosi kutamba juu ya kikosi chake.
Kauli ya Mgosi ni kwamba, timu yake hiyo ina uwezo wa kucheza na Yanga ambayo kesho Jumapili itacheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba, uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti Online, Mgosi amesema kuwaza timu yake kucheza na Yanga ni baada ya kuona ubora wa kikosi cha Simba ambacho kitaivaa Yanga kesho kuwa ni mkubwa na hivyo watani zao lazima wafungwe.
Mgosi alisema katika mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho, Simba ilicheza kwa kiwango cha juu dhidi ya Azam na kupata ushindi wa bao 2-0, hivyo kiwango kile ni kama kuwaonea watani zao.
"Kwa kiwango waliichoonesha Simba dhidi ya Azam, ningekuwa kiongozi wa Yanga nisingeingiza timu uwanjani, au nitaongea na viongozi wa Simba kama itawezekana waandike barua TFF (Shirikisho la Soka nchini), Simba Queens wacheze na Yanga siku hiyo.
"Sijaona ni jinsi gani, maana Simba imeamua kufanya kazi, naamini tutakuwa kama tunawaonea, kutokana na mpira wa Simba, ikiwa Simba watacheza kama vile walivyopanga, nina uhakika mashabiki wa Yanga wataondoka uwanjani mapema, sasa ili hilo lisitokee, lazima wacheze na Simba Queens" aliongeza.