Mgombea Uenyekiti Simba amtaja Mo Dewji

MGOMBEA wa nafasi ya uenyekitiwa klabu ya Simba, Moses Kaluwa amesema iwapo wanachama wa timu hiyo watamchagua atarudisha uhai wa matawi pamoja na kushirikiana na mwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo’.

Kaluwa ambaye ni Wakili anagombea nafasi hiyo na Murtaza Mangungu anayetetea kiti chake.

Akizungumza katika kampeni zilizoandaliwa na wanachama wa klabu hiyo Jijini Dodoma, mgombea huyo alisema kwa sasa mwamko wa matawi kuisaidia timu ni mdogo hivyo kama atachaguliwa atahakikisha anarudisha uhai wa wanachama.

“Endapo nitachaguliwa nitahakikisha tunapata wanachama na mashabiki wengi kupitia kamati nitakayoiunda.

“Inauma haiwezekani timu ikatembea na Coastal lazima tukubali kuna sehemu kuna legalega lazima tupaweke vizuri .Nitashirikiana na wazee ikiwemo kukiboresha chumba namba 4, pale makao makuu ya timu.

“Kuna maneno kwamba mimi sipo tayari kufanya kazi na mwekezaji Mohammed Dewji Mo, naomba niwaambie wanachama na mashabiki wa Simba, naheshimu kile anachofanya mwekezaji na nitashirikiana naye katika kila anachofanya, maneno ya mitaani naomba myapuuze,” alisema mgombea huyo wakati akimwaga sera zake.

Alisema iwapo atachaguliwa atachagua watendaji wenye uzoefu ambao watatoa ushauri wa kuisaidia klabu hiyo kuzidi kupiga hatua.