Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgeveke, Samson wa Mwadui wampoteza vibaya Kagere

Muktasari:

Mabao ya Clatous Chama na Francis Kahata katika kila kipindi yalitosha kuipa ushindi Simba dhidi ya Mwadui FC ambayo ilipata bao lake kupitia kwa Gerrard Mdamu.

Simba imelipa kisasi kwa Mwadui FC baada ya jana kuichapa kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Clatous Chama na Francis Kahata katika kila kipindi yalitosha kuipa ushindi Simba dhidi ya Mwadui FC ambayo ilipata bao lake kupitia kwa Gerrard Mdamu.
Matokeo hayo yameifanya Simba itinge hatua ya 16 bora ya mashindano hayo ambayo ilianzishwa msimu wa 2015/2016.
Ifuatayo ni tathmini ya mchango wa mchezaji mmojammoja kwa timu yake katika mchezo huo wa jana kwa namna ulivyochangia kupatikana kwa matokeo hayo.

Simba
Beno Kakolanya-7
Hakushambuliwa mara kwa mara na Mwadui ila alikuwa imara kuokoa hatari chache zilizoelekezwa langoni mwake mfano shambulizi la ana kwa ana la mshambuliaji Ludovic Evans katika dakika ya 14.

Shomary Kapombe-9
Kasi na uwezo wake vilikuwa ni mwiba kwa Mwadui FC. Alipandisha mashambulizi na kupiga krosi za mara kwa mara, pia pale alipohitajika katika kujilinda alitimiza jukumu hilo kwa ufasaha. Ndiye aliyepiga krosi iliyozaa bao la pili la Simba ambalo liliipa ushindi.

Mohammed Hussein-6
Hakuwa na kasi kubwa lakini alijitahidi kutimiza majukumu ya nafasi yake kwa kusaidia mashambulizi na pia kushiriki katika kujilinda pale walipokuwa wanashambuliwa. Hata hivyo hakuwa katika nafasi sahihi pale Mwadui walipofanya shambulizi kupitia upande wake ambalo lilizaa bao.

Erasto Nyoni-6
Alikuwa na tatizo la kutosimama katika nafasi sahihi pale walipokuwa wanashambuliwa na hakuwa na mawasiliano mazuri na mwenzake jambo lililopelekea waruhusu mashambulizi kadhaa ambayo yangeweza kuzua balaa.

Pascal Wawa-7
Alikosa mawasiliano mazuri na mwenzake Erasto Nyoni jambo lililopelekea mara kadhaa wafanye makosa ambayo pengine yangeigharimu Simba ingawa mara kadhaa alijaribu kuichezesha timu kuanzia nyuma

Jonas Mkude-6
Alifanya kazi kubwa mwanzoni mwa kipindi cha kwanza ya kutibua mipango ya Mwadui, hata hivyo, mara kadhaa aliachia mianya ambayo kama wapinzani wao wangeitumia vizuri ingeleta madhara langoni mwao.

Hassan Dilunga-7
Alifanya vizuri katika kuchezesha wenzake lakini alikosa umakini wa kutumia nafasi ambazo yeye alitengenezewa jirani na lango la adui.
Angeweza kufunga mabao mawili kupitia nafasi mbili za wazi alizopata kipindi cha kwanza lakini zote alizipoteza kwa kupiga mashuti yaliyopaa na lingine kutoka nje.

Sharaf Shiboub-6
Alicheza taratibu lakini kwa umakini wa hali ya juu. Alipiga pasi zilizoonekana kuwa tishio kwa Mwadui na chenga zake ziliweza kuvunja ukuta uliowekwa na wapinzani wao mara kwa mara. Hata hivyo alichoka na kutolewa huku nafasi yake ikichukuliwa na Ibrahim Ajibu.

Meddie Kagere-5
Alikuwa chini ya ulinzi mkali wa walinzi wa Mwadui ingawa mara kadhaa alijitahidi kufurukuta kusaka mabao.
Mfumo wa Simba ulimbana na kujikuta akikosa huduma sahihi ya pasi ambazo angeweza kuzitumia kufunga mabao.

Clatous Chama-8
Alikuwa mwiba hasa katika kipindi cha kwanza kutokana na namna alivyokuwa akitengeneza nafasi, pia mikimbio yake iliwapa shida Mwadui FC.
Alifunga kwa ustadi bao la kusawazisha la Simba mara baada ya kuwatoka walinzi watatu wa Mwadui FC lakini alichoka dakika za mwishoni za kipindi cha pili.

Francis Kahata-7
Muda mrefu alionekana kutokuwa mchezoni kutokana na kupoteza pasi na mipira mara kwa mara hasa katika kipindi cha kwanza huku akichelewa kufanya uamuzi pale alipokuwa na mpira mguuni.
Alifanya kosa la kumsindikiza Ludovic Evans ambaye alipiga pasi iliyozaa bao la Mwadui FC lakini akaja kulirekebisha kwa kufunga bao la ushindi la Simba akimalizia kwa kichwa krosi ya Shomary Kapombe.

Walioingia
Ibrahim Ajibu-3
Pasi zake kadhaa za mwisho alizopiga zilinaswa na walinzi wa Mwadui ingawa alijitahidi kuongeza umiliki wa mpira ambao uliisaidia Simba kulinda ushindi.

John Bocco-5
Alisaidia kuwanyima uhuru walinzi wa Mwadui kutoshiriki katika kujenga mashambulizi pale walipokuwa wanajaribu kusogea mbele kusaka bao la kusawazisha lakini alikosa umakini wa kutumia nafasi na katika dakika za lala salama, alipoteza moja nzuri ambayo ingeweza kuipa Simba bao la tatu.

Mwadui
Mussa Mbisa-7
Alitimiza wajibu wake langoni kwa kuipanga vizuri safu yake ya ulinzi na kuokoa hatari zilizoelekezwa golini mwake na washambuliaji wa Simba.
Hesabu zake zilikuwa sahihi na mabao aliyofungwa hayakutokana na udhaifu wake.

Mfaume Omary-5
Alicheza kwa nidhamu ya hali ya juu katika ulinzi kwa kutopanda mbele mara kwa mara na kubaki nyuma ingawa kwa upande mwingine hiyo ilisababisha winga na beki wa kushoto wa Simba kuvuka mstari wao  mara kwa mara na kuwepo katika nusu yao. Hakupanda mbele kumsaidia winga wake lakini pia hakuwa na kasi.

Halfan Mbaruku-4
Alionekana kupania mechi na kucheza faulo za mara kwa mara hasa kwa Hassan Dilunga na miongoni mwa hizo, mojawapo ilipelekea aonyeshwe kadi ya njano na refa Ahmed Arajiga kutoka Manyara.

Augustino Samson-6
Alimdhibiti vizuri Meddie Kagere na kufanikiwa kuokoa mipira mingi ambayo mshambuliaji huyo alipenyezewa au ambayo Simba waliidondosha katika eneo lao la hatari.

Joram Mgeveke-6
Alitumia vyema umbo lake kuondosha mipira ya juu ambayo Simba waliielekeza langoni mwake, alitoa msaada kwa walinzi wake wa pembeni kila ilipohitajika na alicheza kwa utulivu wa hali ya juu.

Enrik Nkosi-7
Aliilinda safu ya ulinzi ya Mwadui kwa kuziba mianya ya Simba kupenyeza mipira kupitia katikati, alipora mipira na kuitawanya kwa haraka na aliichezesha timu kwa kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi.

Benjamin Sowah-5
Alimpa wakati mgumu beki wake kwa kutoshuka kumsaidia mara kwa mara pale walipokuwa wanashambuliwa lakini pia alichelewa kufanya maamuzi pindi mpira ulipokuwa mguuni.

Charles Ndahaza-5
Alianza vizuri katika robo saa ya mwanzo ya mchezo lakini alijikuta akielemewa na viungo wa Simba na kushindwa kuiunganisha timu hali iliyopelekea Mwadui kukosa balansi katikati mwa uwanja na kuwaruhusu wapinzani wao kutawala mchezo.

Gerard Mathias-7
Hakuwa tishio sana uwanjani ila alikuwa ni mjanja wa kukaa katika nafasi sahihi pindi walipokuwa wanashambulia na hilo lilimsaidia kwa kufanikiwa kuifungia Mwadui bao la kuongoza mnamo dakika ya 35 akimalizia pasi aliyopigiwa na Ludovic Evans

Ludovick Evans-8
Alikuwa mwiba kwa walinzi wa Simba kutokana na kasi na uwezo wake wa kumiliki mpira. Hakupoteza mpira kirahisi pindi ulipokuwa mguuni na alitengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo kama zingetumiwa vyema huenda timu yake ingepata idadi kubwa ya mabao.

Omar Daga-6
Alionekana kutokuwa mchezoni katika kipindi cha kwanza na alifichwa vilivyo na Shomary Kapombe, lakini kipindi cha pili alijitutumua na kujaribu kuongezeka ndani jambo lililoongeza uimara kwa Mwadui katikati mwa uwanja.

Walioingia
Abdul Masikin-3
Hakutoa sapoti ya kutosha kwa Ludovic Evans na hakuonekana kuwa na madhara kwa walinzi wa Simba. Alipoteza mipira mingi aliyopigiwa ambayo ilinaswa kirahisi na mabeki wa wapinzani wao.