Mfaransa wa Tabora United atimka

Muktasari:

  • Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba, kocha huyo aliyetambulishwa Machi 22, mwaka huu ameondoka ikiwa ni baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyopigwa Aprili 17 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Tabora United Mfaransa, Denis Laurent Goavec ameondoka ndani ya timu hiyo ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu ajiunge nayo akichukua mikoba ya Mserbia, Goran Kopunovic aliyetimuliwa Machi 21, mwaka huu kutokana na matokeo mabovu.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba, kocha huyo aliyetambulishwa Machi 22, mwaka huu ameondoka ikiwa ni baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyopigwa Aprili 17 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.

"Ni kweli kocha ameondoka na sababu kubwa ni kutoridhishwa na maendeleo ya klabu yaliyopo, amekuwa haelewani na baadhi ya wachezaji na viongozi hivyo ameona ni vyema kuondoka kwa lengo la kulinda heshima yake," kilisema chanzo chetu.

Mwanaspoti lilimtafuta mwenyekiti wa timu hiyo ambaye pia ni RPC wa Tabora, Richard Abwao aliyeeleza hakuna ukweli wa taarifa hizo.

"Hivi karibuni tuna kikao chetu cha kujadili mambo mbalimbali ya timu na suala la kuondoka kwa kocha kwa kweli hilo halijanifikia mezani kwangu, kikubwa ninachowashauri wapenzi na mashabiki wetu waendelee tu kutuunga mkono," alisema.

Licha ya kauli hiyo, Mwanaspoti linatambua tayari kocha huyo amewaaga wachezaji na kuanzia sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya aliyekuwa kocha msaidizi Mrundi, Masoud Djuma aliyewahi kuzifundisha klabu mbalimbali zikiwemo Simba na Dodoma Jiji.

Goavec alianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate katika hatua ya 16 bora ya ASFC kisha kufuatia sare ya bao 1-1 na JKT TZ, Aprili 13, 2024), kisha kuchapwa mabao 3-0 na Kagera Sugar Aprili 17, 2024 na kuondoka zake.

Kwa upade wa Goran aliyeifundisha Simba hadi anaondoka ndani ya kikosi hicho alikuwa tayari amekiongoza katika michezo 21 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda minne, sare tisa na kupoteza minane akiiacha nafasi ya 13 na pointi 21.