Metacha bye bye Yanga

Saturday June 19 2021
metacha pic2
By Mwandishi Wetu

VIGOGO wa Yanga, wamelihakikishia Mwanaspoti kwamba uwezekano wa kipa wao namba moja, Metacha Mnata kusalia Jangwani msimu ujao ni finyu kama Mwadui kutwaa ubingwa msimu huu.

metacha pic

Hiyo inamaanisha kwamba hakuna uwezekano kabisa wa staa huyo aliyesimamishwa kubaki Jangwani kwani tayari Mwadui anayofananishwa nayo imeshashuka daraja na inakamilisha tu ratiba isepe zake Daraja la Kwanza. Metacha aligeuka habari ya mjini, baada ya kuwaonyesha ishara ya utovu wa nidhamu mashabiki waliokuwa wanamzomea akitoka Uwanja wa Benjamin Mkapa,Yanga ikishinda mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting, kwamba mabao aliyofungwa yalikuwa ni ya kizembe.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba tangu awali walishajua kuwa Metacha ataondoka na walishajiandaa kisaikolojia kusaka kipa mwingine kwani hata Nabi amependekeza kwenye ripoti yake ukiacha nafasi ya beki wa kati, kulia na kushoto.

metacha pic3

Alisema kwamba nidhamu aliyoonyesha Metacha haivumiliki na kwamba wamemsimamisha kwa muda lakini hiyo ndiyo imetoka kwani wakimuacha ataigawa timu kuanzia vyumbani mpaka jukwaani.

Advertisement

Hata hivyo, mchezaji huyo kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii aliwaangukia wanayanga na kuwaomba radhi, ikiwa ni saa kadhaa tangu uongozi wa klabu hiyo kutoa taarifa ya kumsimamisha kwa alichokifanya uwanjani baada ya mchezo huo na kwamba wanampeleka Kamati ya Maadili.

Wadau mbalimbali wamezungumzia ishu ya Metacha juzi huku Kocha mkuu wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa akidai ; “Jambo lake linahitaji watalamu zaidi wa saikolojia ili kumjenga, naamini atarejea kwenye nidhamu yake, hadi anafanya jambo hilo hayupo sawa, pia lazima mashabiki wajue kwamba kipa anakuwa na presha kubwa hivyo anaweza kufanya makosa kama binadamu wa kawaida.”

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alisema mchezaji anapokuwa uwanjani damu yake inakuwa imechemka anakuwa nusu mnyama, hivyo anaweza akafanya jambo lolote baya kama atakosa utulivu wa kukabiliana na mazingira yanayokuja kinyume chake.

Naye Saad Kawemba ambaye aliwahi kuwa Mtendaji mkuu wa Azam, alisema; “Mchezaji anahitaji mashabiki kuliko shabiki anavyomuhitaji mchezaji, Yanga wanaweza kuleta mchezaji mwingine na akavaa jezi kisha akashangiliwa hivyo ndivyo mashabiki walivyo.”

“Uongozi kumsimamisha Metacha ni jambo zuri kwa sababu wanalinda taswira ya timu kwa mashabiki waje uwanjani mechi zijazo, ”alisema huku akiungwa mkono na aliyekuwa meneja wa Azam FC, Philip Alando.

Advertisement