Yanga: Tunaleta majembe

Muktasari:

YANGA wametamba safari hii kwenye usajili wao wanashusha majembe tupu na hawabahatishi kwani wameshajua walichemka wapi.

YANGA wametamba safari hii kwenye usajili wao wanashusha majembe tupu na hawabahatishi kwani wameshajua walichemka wapi.

Msimu uliopita Yanga ilikuwa gumzo baada ya kusajili wachezaji zaidi ya 20 huku wengine wakiachwa katika msimu huu, kitendo ambacho walionekana kukijutia kutokana na timu kukosa muunganiko hadi sasa.

Kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara tayari Yanga wameanza kufanya usajili wa nyota wazawa na wa nje wakiwa na lengo la kuboresha zaidi kikosi chao kiweze kutimiza malengo ya kulitwaa taji hilo.

Akizungumza na Mwanaspoti jana Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro alisema kwa sasa wanajitahidi kuhakikisha wanafanya usajili ambao utakuwa mzuri zaidi ya uliopita.

Alisema lengo ni kuhakikisha kwamba wanarejesha hadhi ya klabu hiyo ndani ya uwanja kwa kufanya vizuri zaidi na kubeba makombe wakianzia na timu ya wakubwa.

Kandoro aliongeza kila wanachokifanya kwa sasa wanafanya kimkakati ndio maana wameamua kuanza mapema kwa kuzingatia maelekezo ya kocha ili kufanya maandalizi ya kina na kuwa kwenye hali nzuri mapema tofauti na misimu ya hivikaribuni.

Aliongeza kuwa wamejifunza kwenye makosa mengi waliyofanya na wanajua kilichotokea hivyo hawatarajii tena kurudia makosa na punde mashabiki na wanachama watawaelewa. Mwanaspoti linajua kwamba tayari Yanga imeshamalizana na Shabaan Djuma wa AS Vita ya DR Congo ambaye ni beki na kiungo mwingine Mcongo,Mercey Vumbi. Dili la Lazarous Kambole wa Kaizer Chief limeshindikana kutokana na dau kubwa la mshahara.

Kwa upande wa wazawa imewasajili David Brayson wa KMC na Dickson Ambundo wa Dodoma Jiji.

Mpaka sasa timu zote za vijana za Yanga zinafanya vizuri iwe U-17, U-20 pamoja na timu ya Wanawake zote zimeleta ushindani zaidi katika michuano ambayo zimecheza.

“U-20 tumeingia nusu fainali, timu ya wanawake ilimaliza ikiwa nafasi ya pili na sasa timu ya wakubwa iko nafasi ya pili inapambania kutwaa taji kwani nafasi bado tunayo,”alisema Kandoro.

Kandoro alisema wanapambana zaidi kuboresha timu za vijana ambazo zitawasaidia zaidi katika usajili siku zijazo ili kuepuka kadhia ya kusaka wachezaji na kutumia pesa nyingi.

“Ukishakuwa na timu nzuri za vijana hata usajili wa timu kubwa haupati sana gharama, na hiyo ndiyo dhamira yetu sisi Yanga ili tuwe na wachezaji wengi na wazuri watakaosaidia timu zetu,” alisisitiza.