Metacha asimamishwa Yanga

Muktasari:

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umemsimamisha kipa wake, Metacha Mnata kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya kwa mashabiki baada ya mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa jana usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umemsimamisha kipa wake, Metacha Mnata kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya kwa mashabiki baada ya mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa jana usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Klabu hiyo imesema kuwa, uongozi umesikitishwa na kitendo kisichokuwa cha kiungwana alichokifanya Metacha hiyo anasimamishwa hadi hapo suala lake litakapofikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya klabu hiyo.


“Kwa kitendo alichokionyeha mchezaji, uongoziu wa Yanga unamsimamisha mchezaji Metacha Mnata kuanzia sasa hadi hapo suala lake litakapofikishwa mbele ya kamati ya nidhamu na kujadiliwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Klabu” imesema taarifa hiyo
Pia, Uongozi umeomba radhi wanachama, wapenzi, mashabiki na wadau wa michezo kwa kitendo hicho alichokifanya Mnata
“Uongozi unaomba radhi kwa wanachama, wapenzi, mashabiki na wadau wote wa michezo kwa ujumla kwa kitendo hicho, uongozi utachukua hatua ya kumpeleka kwenye Kamati ya Nidhamu ya Klabu kwa hatua zaidi” imesema taarifa hiyo nakuongeza
“Aidha uongozi unawaomba wanachama, wapenzi, mashabiki na wadau wote wa soka kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho unalifanyia kazi suala hili kwa mujibu wa taratibu za Klabu”

Kilichotokea kwa Mkapa

Jana usiku baada ya mchezo wa Yanga dhidi ya Ruvu Shooting kumalizika kipa huyo wa Wanajangwani, Metacha Mnata alionyesha ishara mbaya kwa kuwanyoshea vidole mashabiki waliokuwa wakimzomea.
Hiyo ni baada ya Metacha kuzozana na baadhi ya wachezaji wenzake na alipokuwa anaenda vyumbani ndio aliwaonyeshea ishara hiyo kwa mashabiki wa Yanga.
Mashabiki hao ambao hawakufurahishwa na kitendo hicho waliamua kulizunguka gari la timu yao wakimshinikiza kumtaka Metacha aliyetibua furaha yao ya kuifunga Ruvu Shooting
''Tunamsubili aje atuambie kwanini anatuonyeshea vidole kama tusipompata hapa tutamfata nyumbani kwake (akitaja anapoishi mchezaji huyo),” alisikika mmoja wa mshabiki hao.
Hata hivyo shabiki mwingine alipingana na mashabiki wenzake kwa kumtetea Metacha kuwa nae ni binadamu ana moyo wanapaswa waelewe kuwa hakufanya makusudi kutokudaka mpira
''Hawa wachezaji nao ni binadamu tunapaswa kuwaelewa tuwatie moyo sio kuwavunja,” alisema shabiki huyo.
Dakika chache baadae Polisi waliamua kuwafukuza mashabiki hao kwa kutumia mbwa na baadae wachezaji wa Yanga walipanda kwenye basi lao na kuondoka.
Yanga katika mchezo huo wameshinda 3-2 mchezo uliokuwa na ushindani wa hali ya juu kwa dakika zote 90.