Messi vs Ronaldo : Ronaldo ampoteza baba yake akiwa kambi ya ureno

Muktasari:
Ni Jumanne ya Septemba 6, 2005. Siku inayofuata Ureno ilitakiwa kujitupa uwanjani kuvaana na Urusi, hatua muhimu kwa timu yao katika mbio zake za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2006 ambazo mwenyeji alikuwa Ujerumani.
KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi Ronaldo alivyoanza kupiga hatua za awali katika soka utotoni kabla ya kujikuta katika wakati mgumu na kutamani kuachana na maisha ya soka na kurudi nyumbani ili awe karibu na familia. Sasa endelea…
Alihitaji uimara huo katika miaka mingine mingi iliyofuata ili kumsaidia kuendana na kipindi cha huzuni katika maisha yake.
Ni Jumanne ya Septemba 6, 2005. Siku inayofuata Ureno ilitakiwa kujitupa uwanjani kuvaana na Urusi, hatua muhimu kwa timu yao katika mbio zake za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2006 ambazo mwenyeji alikuwa Ujerumani.
Kama wakishinda mechi hiyo na Slovakia kupoteza maana yake, watakuwa hatua nzuri ya kwenda Ujerumani.
Ni saa tatu usiku wakiwa jijini Moscow, Ronaldo alikuwa chumbani kwake akiangalia filamu na Kocha wa timu ya Ureno, Luiz Felipe Scolari alimtaka Ronaldo aende chumbani kwa kocha huyo.
Nahodha wa Ureno, Luis Figo naye pia alikuwa katika chumba hicho kikubwa chenye vitu vyote muhimu, Ronaldo aliona ni jambo la ajabu kidogo kwa yeye kuitwa katika kikao kama hicho, lakini hakuwa amewaza jambo lolote.
Alianza kufikiria itakuwa ni mambo ya mbinu za kiuchezaji jambo ambalo kocha na nahodha wake wangependa kujadiliana naye, lakini ukweli, walimwita kumwarifu kuhusu kifo cha baba yake.
Dinis Aveiro, baba mzazi wa Cristiano Ronaldo alifariki dunia wakati akipata matibabu kwa miezi kadhaa katika zahanati moja ya jijini London, kifo hicho cha mapema mno kilitokana na pombe na kumwacha Ronaldo katika hali ya kuchanganyikiwa.
Hata hivyo, pamoja na hali ya huzuni aliyokuwa nayo, Ronaldo hakutaka kuikosa mechi. “Nataka kucheza, hicho ndicho kitu nilichokijua kukifanya,” alisema baadaye.
“Nataka kumwonyesha kila mtu nilikuwa na uwezo wa kujituliza katika kipindi kigumu na kuweka mambo sawa na mimi ni mwanasoka profesheno na kazi yangu naipa umuhimu, nataka nicheze mechi hiyo kwa heshima ya baba yangu, nataka nifunge bao kwa heshima yake, niko katika kujijaribu mimi na watu wote wanaonipenda.”
Hata hivyo, mechi yao na Urusi ilimalizika kwa sare ya bila kufungana na hakuweza kufunga bao alililotaka kulitoa kama heshima kwa baba yake. Badala yake atafanya hivyo kwenye Kombe la Dunia nchini Ujerumani.
Alifunga bao la penalti katika mechi dhidi ya England na kuipeleka Ureno nusu fainali, aliinua mikono juu mbinguni na akawa kama anasema, “Hili bao ni kwa ajili yako baba.”
Baada ya fainali za Kombe la Dunia zilizoisha kwa Italia kubeba taji, alirudi nyumbani kwao Madeira kwenda kumzika baba yake, alivaa shati jeusi na miwani nyeusi, alikuwa karibu na familia yake na kuonyesha utulivu wake, hakulia lakini macho yake yalionyesha alilia sana hapo kabla.
Siku kadhaa baadaye alizungumzia namna ambavyo vyombo vya habari vilikizungumzia kifo cha baba yake ambacho kilikuwa katika kurasa za kwanza kwa siku nne zilizofuata, “Iliniumiza hasa mimi na familia yangu, tulihitaji amani na utulivu lakini badala yake kilichotokea ni vurugu na hali tete.”
Miaka michache baadaye alimzungumzia Dinis katika namna ya kumshukuru, “Baba yangu wakati wote alikuwa akinihamasisha, alikuwa akiniambia niwe mwenye shauku ya kufanikisha jambo na alikuwa akijivunia maisha yangu ya kucheza soka.
“Ninampenda na nitaendelea kumpenda, wakati wote atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwangu, ningependa kufikiri popote ulipo utaona kile ninachokifanya na kile nilichokifanikisha.
Dinis hakuwa mtu mwenye kupenda kuonekana hadharani, hakuzipenda kamera, alipenda kujiweka nyuma lakini uhusiano wake na mtoto wake kwa wakati wote ulikuwa imara.
Kabla Ronaldo hajaenda Lisbon ilikuwa vigumu kumtenganisha na baba yake, waliendelea kuwa karibu hata alipohamia Manchester, Dinis wakati wote alikuwa naye, alikuwa akimtembelea na kumuunga mkono kwa kumhamasisha hadi alipoanza kuugua.
Mara kwa mara, Ronaldo alikuwa akimwambia baba yake aende hospitali ili kuangalia namna ya kutibu tatizo la ulevi lakini alishindwa kumsaidia, Dinis aliendelea kunywa pombe na ikafikia mahali hakukuwa na la kufanya, hata hospitali zilizo bora England hazikuweza kufanya lolote.
Itaendelea Jumanne ijayo…