Messi akumbuka ubora wa Kim Poulsen

Muktasari:
Kim Poulsen anasifika na ubora wa kutengeneza vijana ambao wamedumu mpaka hivi sasa katika soka la Tanzania
KIUNGO Ibrahim Twaha 'Messi' aliyewahi kuzichezea timu za Taifa chini ya miaka 17 na 20, amejikuta akikumbuka namna vikosi hivyo vilivyokuwa bora miaka ya 2011 mpaka 2013.
Messi ambaye hivi sasa anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 amesema kwamba wakati anachezea timu hizo za vijana ni wazi alikuwa akikuzwa katika njia bora ya soka.
"Nimekuwa na miaka mitatu katika timu ya vijana, kiukweli hii timu iliboresha uwezo wangu hasa mwalimu Kim Poulsen, ni kocha bora kwangu kwa muda wote," aliyazungumza hayo leo kwa njia ya simu akiwa nyumbani kwao Dar es Salaam.
Messi amesema timu hiyo ilikuwa bora kutokana na kuingia kambini kila mwezi kwa wiki mbili na kupishana na timu ya juu yao tofauti na ilivyo hivi sasa.
"Mara nyingi tulikuwa tukiingia kambini ndani ya mwezi kwa wiki mbili tukipishana na timu ya chini miaka 20, kipindi kile walikuwemo akina Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Hassan Kessy, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Atupele Green, Lambele Jerome na hata Aishi Manula ambaye alikuwa na sisi lakini kocha Kim akampeleka juu yetu,".
Aliongeza kwa kusema vijana wote waliokuwa kipindi hicho walikuwa wakipanda polepole kutoka miaka 17 kwenda 20, 23 mpaka timu ya Taifa kubwa.
"Ilikuwa ni zaidi ya akademi na ndio maana vijana waliopita kwenye mikono ya Kim Poulsen leo hii wote wamepata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara na nje ya nchi " amesema nyota huyo ambaye yupo huru hivi sasa.
Serengeti Boys ikiyofundishwa na Kim imewatoa nyota wengi wanaocheza Ligi Kuu mpaka sasa.
Lakini kocha huyo aliondoka nchini baada ya mkataba wake kumalizika licha ya kudumu takribani miaka nane nchini.
Kim alianza kufanya kazi mwaka 2011 akiwa na timu huyo ya vijana na mwaka 2014 alipewa timu ya wakubwa ya Tanzania 'Taifa Stars' lakini aliondolewa baada ya kufanya vibaya.
Mwaka 2016 alirejea na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na kudumu kwa miaka miwili tu (2018) alipokuwa akisaidiana na Oscar Milambo ambaye hivi sasa ndio anayeshikilia nafasi hiyo.
Kim hivi sasa yupo nyumbani kwao Denmark akiendelea na shughuli zake nyingine.
Messi pia licha ya kucheza timu hizo, alipata kucheza katika klabu za Simba, Coastal na Kagera Sugar na hivi sasa ni mchezaji huru baada ya kutosajili sehemu yoyote.