MEDDIE KAGERE: Mechi ya Al Merreikh ngumu, ila tumepania kuwanyoosha kwao

TUNASHUKURU tumefika salama Sudan baada ya safari ndefu kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wetu wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wetu, Al Merreikh.

Mchezo huu utapigwa Jumamosi (kesho) na kwa hakika lazima nikiri, tutakuwa na mechi ngumu kuliko mbili tulizocheza dhidi ya AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri, tofauti na wengi wanavyouchukulia mchezo huo.

Kama mchezaji huwa najua namna inavyokuwa unapokabiliana na timu iliyopoteza michezo miwili mfululizo. Al Merreikh ilipoteza mechi zao za awali katika hatua hii ya makundi na hii ndio inayoufanya mchezo huu kuwa mgumu.

Wapinzani wetu wamepoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Al Ahly ambayo ni timu kubwa na jambo hilo halina kubishi.

Baada ya hapo walirudi nyumbani kwao kucheza na Vita wakapoteza kwa mara nyingine, hivyo ni wazi hawatakubali kufungwa tena nyumbani kirahisi.

Wakati wao hawatakubali kufungwa nyumbani, wanakutana na Simba ambayo mechi zetu mbili za awali tumeshinda.

Ndio sababu nasema wataingia na nidhamu kutokana kwamba wanacheza na vinara wa kundi.

Mchezo utakuwa mgumu kutokana na sababu hiyo lakini hawa Al Merriekh wanamfahamu kocha wetu ambaye ameshawahi kufanya kazi kwao.

Kuna faida ambayo itakuwa kwa upande wetu kutonakana na jambo hilo la kocha wetu kuwafahamu lakini hata wao nao watafaidika nao kwa kumjua kocha wetu.

Tunatambua tunakuja kucheza ugenini kwa maana hiyo tutakuwa na nidhamu ya hali ya juu katika mchezo wetu kwa kuwapa heshima wapinzani.

Ukiangalia mechi ambayo tutacheza huku mbinu zake hazitakuwsa kama zile ambazo tulizifanya katika mechi iliyopita Dar es Salaam, tukicheza na Ahly.

Lakini kuna jambo jingine kwa upande wangu nimeshawahi kuja kucheza mechi Sudan nikiwa na Gor Mahia.

Nakumbuka mechi hiyo tulifungwa bao 1-0, lakini kuna vitu ambavyo nilijifunza na nitakwenda kuvitumia wakati huu na kutoa msaada kwa timu yangu ili kupata matokeo mazuri.

Unajua mechi hizi za ugenini zinahitaji mambo mengi ili kushinda au kupata hata pointi moja ambayo utatuweka katika mazingira mazuri kuliko kukosa kabisa.

Unajua wakati huu timu yetu inaongoza msimamo wa kundi, kwa maana hiyo kila timu itakuwa kucheza kweli bila masihara ili kutupunguza kasi.

Jambo la kupunguza kasi kwa maana ya kushindwa kupata pointi hatutamani kuona linatokea kwa upande wetu ndio maana tumejipanga kikamilifu.

Suala jingine tumepata muda wa kuwangalia Al Merriekh wakicheza na Al Ahly walikuwa wakijilinda zaidi kuliko kushambulia.

Katika kujilinda kwao huko walikuwa wakifanya makosa mengi ambayo Al Ahly waliyatumia na kuwafunga mabao matatu.

Walikuja kubadilika katika mechi hao ya nyumbani walipocheza na As Vita kwa kushambulia lakini jambo hilo halikuwa na faida kwani walifanya makosa mengi zaidi wakafungwa.

Mechi dhidi yetu ambayo wanacheza nyumbani tena inaweza kuamua kwamba watakuwa katika mbio za kwenda robo fainali au wataishia hapo.

Ni wazi watakuja kwa kushambulia na kutaka kutofungwa ili kupunguza presha ambayo wanayo lakini naamini tutafanya vizuri.

Kama tutafanikiwa mipango yetu ya kupata bao la kwanza mapema katika mchezo tunaweza tukawavuruga na tukapata kile ambacho tunahitaji kutoka kwao.

Naamini watakuwa wakicheza huku wakiwa na presha wakati huo nasi tunaangalia namna ya kuwazuia na kuwashambulia.

Kikubwa mechi itakuwa ngumu ila maandalizi na hali pamoja na morali ya timu tunaimani tutarudi na matokeo mazuri.

Kikubwa tunaomba mashabiki na wapenzi wetu wazidi kutuombea ili tupate tunachokitaka huku Sudan.