Mechi ya Stars na Tunisia yapigwa kalenda

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kusogeza mbele kwa mechi ya Taifa Stars dhidi ya Tunisia, ambayo awali ilipangwa kupigwa Novemba 9, sasa rasmi itakuwa Novemba 13 nchini Tunisia.

Stars kabla ya kukutana na Tunisia Novemba 13 kwenye michuano ya kufuzu fainali za CHAN, itajipima ubavu na mechi ya kirafiki ya kimataifa na Burundi siku ya Jumapili, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TFF kupitia taarifa yao walioisambaza kwa vyombo vya habari imesema mechi ya marudiano ya Stars na Tunisia itapigwa Novemba 17, jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kutoka kwa ratiba hiyo kuliibuka mijadala mitandaoni ikihoji mabadiliko ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyosogezwa Novemba 7 badala ya Oktoba 18 kuingiliana na mechi hiyo ya kimataifa

Kikosi cha Stars, tayari kimeishaanza mazoezi tangia jana Jumanne ya Oktoba 6, ambapo Nadir Haroub 'Cannavaro' alieleza kwamba wachezaji wana morali na hamu ya kucheza mechi ya kirafiki kujiandaa na Tunisia.

"Kila mchezaji anatamani kuonyesha kiwango ili kupata nafasi ya kucheza mechi ya Tunisia, hivyo kocha ndiye mwenye jukumu kubwa lakujua nani atafanya nini hasa baada ya kuwaangalia kupitia mechi ya kirafiki na Burundi,"amesema Cannavaro.