Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi tatu za Simba zawapa jeuri Geita Gold

BENCHI la ufundi la Geita Gold limesema limepata muda wa kutosha wa kuitazama na kuisoma Simba katika michezo yake mitatu ya viporo jambo ambalo limewasaidia kupata mbinu na njia bora za kuizuia na kupata ushindi katika mchezo wa kesho Jumatatu.

Geita Gold itakuwa mwenyeji wa Simba kesho kuanzia saa 10:00 Alasiri katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kwenye mchezo namba 101 wa Ligi Kuu.

Akizungumza leo Februari 11, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza, Kocha msaidizi wa Geita Gold, Lucas Mlingwa amesema wamewaandaa wachezaji wao vizuri kisaikolojia na kiufundi baada ya kufuatilia Simba, hivyo anaamini watapata matokeo mazuri kesho.

Mlingwa amesema wachezaji wote wa kikosi hicho wako kamili kuivaa Simba, isipokuwa nahodha, Elias Maguli ambaye bado hana uhakika kutokana na majeraha ya muda mrefu yanayomsumbua, huku wakiisubiri ripoti ya mwisho ya daktari kabla ya kesho ili kupata uhakika zaidi.

"Ni kweli hatujacheza muda mrefu lakini wakati wao (Simba) wanacheza sisi tulikuwa tutafanya maandalizi huku tukitazama wanavyocheza, kwa hiyo tunajua mwenendo wao. Tumepata mechi mbili za kirafiki mwalimu ameona kikosi chake, hivyo hakutakuwa na kisingizio chochote," amesema Mlingwa na kuongeza;

"Tumeandaa timu yetu vizuri kisaikolojia na kiufundi kulingana na mpinzani wetu anachezaje, tumebahatika kuona michezo yake ya karibuni hiyo ni 'advantage' kwetu tuko sawa na tayari kwa mchezo, tunakwenda kupambana kupata matokeo, mechi hii imekuja wakati mwafaka."

Akizungumzia kutopata ushindi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba katika michezo iliyopita dhidi ya Yanga na Simba, Mlingwa, amesema "Sisi CCM Kirumba ni uwanja wa nyumbani, tunakwenda pale kifua mbele na kucheza kwa tahadhari kubwa kutokana na matokeo ya sasa ya Simba na nafasi waliyopo lakini tunajivunia pale ni nyumbani tunaingia tukiwa na ari na nguvu kubwa ya kupambana."

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Elias Maguli, amesema wanachokihitaji katika mchezo huo ni matokeo ya alama tatu katika uwanja wa nyumbani kwani wachezaji wanafahamu Simba ni timu ya aina gani na wamepata muda mzuri wa kujiandaa chini ya kocha mpya Denis Kitambi, hivyo, wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo.

"Tunachokwenda nacho kesho ni mpango wa mwalimu na kile ambacho tutakuwa nacho kulingana na namna ambavyo tumewatazama katika mechi zao kama hawatakuwa wamebadilika katika mipango yao kulingana na mechi ambazo tumewatazama," amesema Maguli.