Mechi inayofuata baada ya kipigo kikubwa -3

Muktasari:

  • Hii ni mechi ya kwanza tangu Yanga wawape watani wao Simba kipigo kikubwa cha 5-1, Novemba 5, 2023.

TUNAENDELEA na simulizi zetu za mechi ijayo ya watani wa jadi, Aprili 20 mwaka huu…yaani Jumamosi hii!

Hii ni mechi ya kwanza tangu Yanga wawape watani wao Simba kipigo kikubwa cha 5-1, Novemba 5, 2023.

Hiki ni moja ya vipigo vikubwa ambavyo vimewahi kutokea kwenye mechi watani.

Kupitia makala hizi tunakuletea kumbukumbu ya mechi iliyofuata baada ya kipigo kikubwa kama hiki.

Kuna vipigo vikubwa vinne tu ambavyo vimewahi kutokea.


Yanga 5-0 Simba - 1968

Simba 6-0 Yanga - 1977

Simba 4-1 Yanga - 1994

Simba 5-0 Yanga - 2012

Yanga 5-1 Simba - 2023


Tumekuletea simulizi za mechi zilizofuata baada ya kipigo cha 5-0 cha mwaka 1968 na 6-0 cha 1977.

Leo tunakuletea simulizi ya mechi iliyofuata baada ya mechi ya kipigo cha 4-1 cha 1994.

Dhahama hiyo ilitokea Julai 2, 1994 katika Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru. Bao la kwanza la Simba na lile pekee la Yanga yalıfanana sana.

Yote yalitokana na mikwaju ya adhabu ndogo na yote yalifungwa na walinzi wa kati.

Bao la Simba lilifungwa na George Masatu na la Yanga lilifungwa na Constantine Kimanda.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Athuman Abdallah ‘China’, ambaye alihamia Simba akitokea Yanga, Madaraka Seleman na Dua Said.

Tofauti na mechi zingine zilizofuata baada ya kipigo kikubwa tulizozijadili huko nyuma, mechi iliyofuata baada ya hapa haikuwa mbali sana. Ilichukua miezi minne tu kuja mechi hiyo iliyofanyika Novemba 2, 1994.

Hii ilikuwa mechi ya Ligi ya Muungano, ambayo ndiyo ilikuwa Ligi Kuu ya Tanzania wakati huo.

Ligi ya Muungano ilianza 1982 ikishirikisha timu bora za juu kutoka Ligi ya Bara na Ligi ya Zanzibar.

Wawakilishi wa Tanzania kimataifa walipatikana kupitia mashindano haya. Bingwa alienda kushiriki Klabu Bingwa Afrika, mshindi wa pili alienda kushiriki Kombe la Washindi na wa tatu alıshiriki Kombe la CAF.

Mashindano haya hayana uhusiano wala ufanano wa kihadhi na Ligi ya Kombe la Muungano litakaloanza mwaka huu.

Hili la sasa ni Kombe la Muungano, ile ilikuwa Ligi ya Muungano.

Idadi ya timu zilizoshiriki Ligi ya Muungano ilibadilika mwaka hadi mwaka kutokana na matakwa ya waandaaji.

Mwaka huo, 1994, kulikuwa na timu sita, tatu kutoka Bara na tatu kutoka Zanzibar. Watani wa jadi, Yanga na Simba walikuwa miongoni mwa timu tatu za bara.

Sasa Novemba wakakutana na ikawa nafasi kwa Yanga kulipa kisasi.

Lakini hata hivyo, Simba walikuwa katika wakati bora sana kwani kikosi cha kilitoka kucheza fainali ya Kombe la CAF mwaka mmoja nyuma, na mwaka huo kiliingia robo fainali ya klabu Bingwa Afrika.

Yanga hawakuwa kwenye wakati mzuri kwani walikuwa na mgogoro mkubwa sana wa Yanga kampuni na Yanga asili.

Pande hizi mbili zilitofautiana mawazo juu ya kuendesha klabu kisasa. Yanga kampuni lilikuwa kundi la watu waliotaka mabadiliko kwa kukaribisha wawekezaji wenye pesa kuwekeza klabuni.

Yanga Asili walikuwa wale waliopinga wazo hilo, wakitaka klabu yao iendeshwe kama ambavyo imekuwa ikiendeshwa tangu na tangu.

Mgogo huu ukiwagawa sana, kuja kutahamaki ndiyo wakala za uso, nne safi.

Kwa hiyo mechi ya Novemba 2 ingekuwa ya kulipia kisasi…lakini wapi.

Simba wakashinda tena mchezo huo kwa bao 1-0 lililofungwa na Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’ ambaye mwaka huo ni kama alikuwa amewakodi Yanga kwa sababu aliwafunga kama alivyotaka.

Kwa hiyo wakashindwa kulipa kisasi mbele ya Simba.