MDAMU: Ilibaki kidogo tu nijiue kwa kisu

Straika wa Polisi Tanzania, Gerald Mdamu.
KWA sasa uso wa straika wa Polisi Tanzania, Gerald Mdamu umejaa na tabasamu nzito, kinywa chake kinashukuru Mungu, kutokana na hatua kubwa ya maendeleo ya miguu yake, tangu alipopata ajali Julai 9, 2021.
Mwanaspoti limemtembelea nyumbani kwake Tabata, limeshuhudia furaha ya Mdamu, anayetembea kwa msaada wa magongo tofauti na awali alivyokuwa analala kitandani na uso wake ukiwa umejaa machozi.
Mdamu anafunguka mengi usiyoyajua baada ya kuhojiwa na gazeti hili, ikiwemo na namna alivyotaka kujiua na kisu kisa kuzidiwa na maumivu makali.
HALI YAKE
Mdamu anasema japokuwa mguu wake wa kushoto bado ni mzito kuunyanyua, alipofikia anamshukuru Mungu na anajisikia amani ya siku moja kurejea dimbani.
“Ninaweza kusimama bila magongo kwa dakika 20 ila siyo kupiga hatua kwani naanguka kutokana na mguu wa kushoto kuwa mzito na kimebakia kidonda ambacho hakijakauka,” anasema Mdamu na kuongeza;
“Nina sababu ya kumshukuru Mungu na Watanzania, waliojitoa kwa hali na mali hadi hatua hii niliyofika, mguu kwa sasa unahisi tofauti na mwanzo nilikuwa sisikii chochote.”
Anasema anaendelea na matibabu yanayompa mwanga wa kupona kabisa na kuamini ipo siku atarejea uwanjani kwa kishindo kikubwa.
“Acha Mungu aitwe Mungu, nina uwezo wa kubebwa na bodaboda nikaenda Uwanja wa Twiga kuangalia mazoezi wanayofanya wenzangu, kuna wakati najikuta na huzuni na kutamani ningekuwa mzima ningekuwa nacheza, ila yote katika yote nina hatua kubwa sana.” anasema Mdamu na kuongeza;
“Hakika nimejifunza kuishi na watu vizuri na kujua nidhamu ni kitu muhimu katika maisha, kuna wakati nafuatwa na mashabiki wananiambia ungekuwa na kiburi tungekuacha kama ulivyo, wananipa msaada mkubwa kila ninapopita.”
NYUMA YA USHINDI WA POLISI
Mechi ya Machi 15, Azam FC ikichapwa bao 1-0 dhidi Polisi Tanzania Uwanja wa Azam Complex Chamazi, nyuma ya ushindi huo Mdamu alihusika.
“Niliwaambia mkinitoa hapa nyumbani hakikisheni mnashinda vinginevyo msije mkanisababishia matatizo makubwa, kisha tukaondoka kuelekea uwanjani nikapanda gari la wagonjwa na baadhi ya viongozi.” anasema na kuongeza;
“Kipindi cha kwanza timu yangu ilipata bao, wakati wa mapumziko nikaingia vyumbani nikawaambia ndugu zangu naomba mlinde bao, vinginevyo msije mkanisababisha nikadondoka kwenye machuma, wakasema tutapambana kwa ajili yako, wakatimiza ahadi hiyo.”
Anasema wakati anaagana na wachezaji wenzake alijikuta anashikwa na huzuni, kwani alitamani wangeendelea kupiga naye stori ama kwenda nao kambini.
ALITAKA KUJICHOMA NA KISU
“Kuna siku nilijisikia maumivu makali mno, mbele yangu kulikuwa na kopo la dawa ya mbu nikaliminya hadi likabonyea kisha nikalibamiza ukutani, mbele yangu nikaona kisu wakati najivuta nikakichukue ili nijiue mke wangu akaniwahi na kunikumbatia,” anasema Mdamu kwa hisia kali.
Anasema anakumbuka mke wake alimwambia kama Mungu hakuruhusu kifo wakati wa ajali yake, basi anapaswa kuwa mvumilivu na kushukuru.
“Kitu kingine ambacho kilinisaidia sikuwahi kuamini ni ajali ya ushirikina, niliamini imetoka kwa Mungu, kwasababu nilikuwa nasikia mengi kwamba lile eneo watu wakivunjika hawaponi,” anasema.
LUSAJO VS MAYELE
Anasema anafuatilia kila kinachoendelea Ligi Kuu Bara, huku akivutiwa na ushindani wa kufunga mabao uliopo baina ya Reliants Lusajo (Namungo) na Fiston Mayele (Yanga)
“Kama Lusajo hatapata majeraha ana nafasi kubwa ya kuchukua kiatu cha dhahabu, anajua kupambana kulingana na timu aliyopo hawezi kutengenezewa asisti nyingi kama Mayele.” anasema Mdamu na kuongeza;
“Yanga iombe Mungu sana Mayele asiumie kwani ndiye anayeamua matokeo, unaona anapokosekana hata mechi za kirafiki wanayumba, kwanini sijasema anachukua kiatu ana watu wengi wa kumtengenezea asisti hivyo hadi sasa angekuwa na mabao mengi kuliko Lusajo.”
STAILI YA KUSHANGILIA
Anasema kwa sasa anavutiwa na staili ya ushangiliaji ya Mayele, kwamba kuna wakati anajikuta anasahau baadhi ya mambo.
“Nilikuwa nafundishwa kushangilia na mke wangu, ila nina aibu sana mara nyingi ilikuwa inaishia moyoni tu, zaidi nilikuwa nakimbilia kwenye kibendera.”anasema.
UPENDO WA KWELI
“Namshukuru sana mke wangu, amepitia mengi alikuwa na mtoto mdogo, wakati huo huo na mimi niligeuka mtoto kwani alikuwa anafanya kila kitu nikiwa kitandani, nimejifunza kitu kwake,” anasema.
Mdamu alipata ajali Julai 9 mwaka jana akiwa na kikosi cha Polisi wakitoka mazoezini na kuvunjika miguu yote miwili na kuwahishwa KCMC kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Moi.
Kwa muda wa takriban miezi nane ameanza kutembea kwa kutumia magongo, lakini akiwa na furaha na amani na amelishukuru sana Mwanaspoti, klabu yake na wadau wengine wote waliokuwa bega kwa bega hadi kufikia sasa.