MCL yazindua mwongozo wa matumizi ya AI
Muktasari:
- Mwongozo huo unaweka misingi, kanuni na viwango vya usimamizi vitakavyoongoza matumizi yenye uwajibikaji ya AI katika uandishi wa habari, ushirikishwaji wa hadhira, uzalishaji wa maudhui na mifumo ya kazi ndani ya chumba cha habari.
KAMPUNI ya Mwananchi Communications (MCL), imezindua mwongozo wa matumizi ya akili unde (AI), katika shughuli zake za uhariri na uendeshaji wa majukwaa yake mbalimbali.
Mwongozo huo unaweka misingi, kanuni na viwango vya usimamizi vitakavyoongoza matumizi yenye uwajibikaji ya AI katika uandishi wa habari, ushirikishwaji wa hadhira, uzalishaji wa maudhui na mifumo ya kazi ndani ya chumba cha habari.
Akizungumzia uzinduzi huo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Mpoki Thomson, amesema sekta ya habari ipo katika kipindi kikubwa cha mabadiliko ya kiteknolojia, jambo linalofanya taasisi za habari kuwa na wajibu wa kukumbatia ubunifu, huku zikilinda misingi ya uhariri na imani ya umma.
“Akili unde tayari inabadilisha namna habari zinavyopatikana, kuzalishwa, kusambazwa na kutumiwa duniani. MCL tunaiona AI kama nyenzo ya kuimarisha uandishi wetu wa habari, kuongeza ufanisi wa chumba cha habari na kusaidia ubunifu, huku uamuzi wa kibinadamu, uhakiki wa taarifa, maadili na uwajibikaji wa uhariri vikiendelea kuwa msingi wa kila tunachochapisha,” alisema Thomson.
Mwongozo huo unaruhusu matumizi ya zana za AI kusaidia utafiti, uchambuzi wa taarifa, tafsiri, uchakataji wa takwimu, uelewa wa mahitaji ya hadhira, ugunduzi wa maudhui pamoja na kuongeza ufanisi wa mifumo ya kazi.
Kupitia mwongozo huo, maudhui yatakayosaidiwa na AI yataendelea kufanyiwa uhakiki na usimamizi wa kiuandishi, huku uwazi, ulinzi wa faragha, usawa na uwajibikaji vikipewa kipaumbele katika utekelezaji wake.
Mwongozo huo pia unaweka msisitizo katika mafunzo endelevu kwa wafanyakazi na uelewa wa matumizi ya AI kadri teknolojia hiyo inavyoendelea kukua.
Mwananchi Communications Limited (MCL), ni moja ya kampuni zinazoongoza katika sekta ya habari nchini Tanzania ikichapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, pamoja na kuendesha majukwaa mbalimbali ya kidijitali.