Mcheza gofu Nathwani hashikiki Arusha Open

Muktasari:
- Juzi Jumamosi, nyota huyo aliishangaza familia ya gofu kwa kuleta alama bora ya mikwaju 69 ambayo inazidi kiwango cha uwanja cha mikwaju 72 kwa fimbo tatu.
MSHINDI wa raundi ya tatu ya Lina PG Tour, Jay Nathwani anazidi kuwa tishio katika mchezo wa gofu baada ya ustadi wake kuonekana tena katika mashindano ya wazi ya Arusha Open yaliyomalizika jana katika viwanja vya Gymkhana jijini Arusha.
Juzi Jumamosi, nyota huyo aliishangaza familia ya gofu kwa kuleta alama bora ya mikwaju 69 ambayo inazidi kiwango cha uwanja cha mikwaju 72 kwa fimbo tatu.
Ukichanganya na mikwaju 79 ya siku ya kwanza, Jay Nathwani ambaye ni mkazi wa Arusha, aliweza kuongoza kwa mikwaju miwili zaidi ya mpinzani wake wa karibu, George Sembi wa klabu ya TPC ya Kilimanjaro.
Hadi kufika mwisho wa mashimo 36, Nathwani alikuwa akiongoza kwa alama +2 wakati Sembi akimfuatia na alama +4.
“Namshukuru Mungu kwa kucheza vizuri siku ya leo, natumai nitafanya vizuri hata siku ya mwisho kesho,”alisema Nathwani ambaye pia ni mmoja wa wachezaji wa timu ya taifa ya gofu ya Tanzania.
Mchezaji Isiaka Daudi Mtubwi kutoka Klabu ya Lugalo ya jijini Dar es Salaam pia anaendelea kufanya vizuri katika viwanja vya gofu kwa kukamata nafasi ya tatu akiwa na alama +7 ambayo ni mikwaju mitano nyuma ya Nathwani.
Mtubwi ambaye alishika nafasi ya nne katika mashindano ya Lina PG Tour yaliomalizika jijini Arusha juma lililopita, ni mmoja wa vijana wadogo wanaoukuja juu katika mchezo wa gofu kwa miaka ya karibuni.
Moja ya watu waliopata matokeo mazuri kwa upande wa wanawake ni Vicky Elias ambaye ameonyesah kiwango bora katika mashindano haya kwa kuwa katika nafasi ya tisa kati ya wachezaji 48 nyota waliosajiliwa kwa mashindano haya.
“Nimepambana sana hadi kufikia hapa kwani ninacheza na wapinzani wa kike na kiume wenye viwango bora,” alisema Elias baada ya kumaliza mchuano wa mashimo 36 ya siku ya pili ya mashindano hayo.
Arusha Open ni mashindano ya wazi ya ngazi ya kitaifa na yameratibiwa na chama cha gofu nchini(TGU) kwa kushirikiana na waandaji, klabu ya Gymkhana ya Arusha.
Mshindi wa jumla ya mashindano haya ambayo huchezwa kwa mzunguko katika viwanja vya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro na Iringa hutawazwa kuwa bingwa wa taifa katika mfumo wa ubora wa jumla uitwao Order of merits.