Mbuyu Twite akili mingi Yanga

Mbuyu Twite
Muktasari:
- Katika mechi za hivi karibuni Twite amecheza kama beki wa kulia, beki wa kati, beki wa kushoto na kiungo mkabaji kutokana na maeneo hayo kukosa wachezaji kutokana na majeraha pamoja na matatizo mengine.
KIRAKA Mbuyu Twite amefanikiwa kuwazidi ujanja wachezaji wote wa Yanga kutokana na kumudu kucheza nafasi tano tofauti ndani ya uwanja jambo ambalo hakuna mchezaji mwingine wa timu hiyo anayeweza kulifanya.
Twite ambaye alisajiliwa na Yanga kama beki wa kulia miaka minne iliyopita sasa amefanikiwa kucheza katika nafasi zote za ulinzi na kuwa mchezaji ambaye anatumika zaidi katika kikosi cha timu hiyo hasa kunapokuwa na uhitaji maalumu.
Katika mechi za hivi karibuni Twite amecheza kama beki wa kulia, beki wa kati, beki wa kushoto na kiungo mkabaji kutokana na maeneo hayo kukosa wachezaji kutokana na majeraha pamoja na matatizo mengine.
Katika michezo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Twite alicheza kama beki wa kushoto dhidi ya TP Mazembe kutokana na Oscar Joshua kuumia wakati ambao Mwinyi Haji alikuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyokuwa amepata kwenye mchezo dhidi ya MO Bejaia.
Katika mchezo dhidi ya Medeama, Twite alicheza kama beki wa kulia baada ya Juma Abdul kuumia kabla ya baadaye kuchezeshwa kama beki wa kati katika mchezo dhidi ya TP Mazembe ugenini kutokana na mabeki wengine kuwa na matatizo mbalimbali ikiwemo majeraha. Hiyo inamaanisha anafiti karibu kila eneo.