Mbona hawa mapro 10 sio ishu kabisa!

Muktasari:
Sasa hapa Mwanaspoti linakupa dondoo ambazo zinachambua faida na hasara za uwepo wa mapro wa kigeni. Si unajua namba huwa hazidanganyi, tiririka mwenyewe hapa.
MASHABIKI huko mitaani wamegawanyika, ishu ni kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ya kutoridhishwa na idadi ya nyota 10 wa kigeni kusajiliwa timu moja na kupata nafasi ya kucheza wote kwa mpigo.
Dk Mwakyembe alikwenda mbali na kudai, angependa kuona msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, mapro wa kigeni watano tu ndio wanacheza mchezo mmoja ili kulinda vipaji vya wazawa ambao ni tegemeo la Taifa Stars.
Pia, akakazia suala hilo baada ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye kuzungumzia hilo na kutaka klabu kubwa ikiwamo Yanga kurejesha mtindo wao wa zamani wa kuwa na timu za watoto na vijana ili kuwa vikosi imara vya wazalendo.
“Msimu ujao nataka kuona sheria zinabadilika hasa kwa wachezaji wa kigeni, hata ukisajili wachezaji 100 hatuna tatizo ila watakaocheza uwanjani wasizidi watano ama wanne na nitalisimamia hili,” alisema Dk. Mwakyembe.
Lakini, kauli hiyo ikapokewa tofauti na wadau wa michezo baadhi wakimuunga mkono na wengine wakimpinga wakisema idadi hiyo ya mapro haina madhara kwa soka la Tanzania na zaidi inaongeza mzuka.
Sasa hapa Mwanaspoti linakupa dondoo ambazo zinachambua faida na hasara za uwepo wa mapro wa kigeni. Si unajua namba huwa hazidanganyi, tiririka mwenyewe hapa.
WANA MZUKA KINOMA
Inawezekana ni kweli Mapro ndani ya klabu za soka nchini wanakwamisha nyota wazawa, lakini mzuka walionao ni moja ya faida ya vijana wa Kitanzania kujifunza kitu katika maisha ya soka na kufikia mafanikio ya ndoto walizonazo.
Soka ni ajira kwa sasa na mchezaji wa kulipwa hapaswi kubembelezwa, kudekezwa ila ni wajibu wake kuwajibika kwa vile wanasajiliwa na kulipwa mamilioni ya fedha kufanya kazi.
Wageni wanalijua hilo, wamelelewa namna hiyo ndio maana licha ya kuja wakiwa tayari umri umewatupa mkono, lakini moto wanaouwasha unawafanya iwe ngumu kwao kuachwa benchi na makocha wa klabu wanazozichezea.
Kadhalika wachezaji wazawa na hasa vijana ni fursa ya kujifunza mambo mengi ikiwamo mbinu na ufundi ambazo wageni wamekuwa nazo na jinsi wachezaji hao walivyo na nidhamu kwenye suala zima la kuzitumikia timu zao kwa kutambua wapo kazini. Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Clatous Chama, Donald Ngoma, Yakub Mohammed na wageni wengine wana vitu ambavyo wazawa wakijifunza wanaweza kuongeza kitu na kupambana kwa jasho na damu uwanjani.
MBONA SIO TATIZO
Ishu kubwa ambayo inaweza kuisaidia Tanzania ni kuhakikisha tunahamasisha wachezaji wengi hasa chipukizi wanatoka kwenda kucheza soka nje ya nchi kama yalivyo mataifa mengine kama DR Congo, Zambia, Kenya, Afrika Kusini na hata Ulaya ikiwezekana.
Kama ni kweli wageni ni kikwazo cha mafanikio, tupige hesabu nyepesi tu, klabu za Simba, Yanga na Azam ndio ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikichuana kusajili nyota wa kigeni na katika hesabu ndogo klabu hizo tatu huwa zinasajili wachezaji wasiozidi 30.
Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kwa sasa ni 20 na kanuni zipo wazi kuwa klabu inapaswa kusajili wachezaji wasiozidi 30 na tufanye klabu zote kila moja inasajili wachezaji 27, maana yake ni kwamba msimu mzima Ligi inakuwa na nyota 540.
Katika hao 540, tuwaondoe 30 wa kigeni waliopo klabu kubwa za Yanga, Simba na Azam ambao hesabu yake itakuwa ni kama wachezaji 510 ambao ni wazawa waliopo klabu hizon kubwa na nyingine 17, hapo madhara yao yapo wapi?
Katika wageni hao 30 na ushei, kuna baadhi yao hawana namba za kudumu vikosini hivyo kutoa nafasi kwa wazawa. Madhara yanatoka wapi hapa hadi makocha kushindwa kupata wachezaji wa kuunda Taifa Stars matata?
Kadhalika ujio wa wageni katika soka la Bongo na klabu zetu ni msaada kwa timu hizo. Kwa mfano rekodi za hivi karibuni zinaonyesha Yanga imefika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili 2016 na 2018, huku Simba ikiongozwa na kina Kagere, Chama na Okwi walifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika? Tutafakari tu!
WAZAWA WANAJIKABA
Kwa kuangalia hilo ni wazi kuna tatizo mahali, lakini halitakiwi kusemwa juu ya kuanguka kwa soka la Tanzania na kupotea kwa nyota wazawa katika anga za kimataifa.
Kama nilivyoeleza hapo juu, wazawa wanaachwa mbali na wageni kwa kushindwa kujua wapo kwenye soka kwa sababu zipi? Wanachukulia kucheza kwao soka ni kama fasheni na sio kazi na ndio sababu hawapendi mazoezi, wana masihara na hawajitoi kwa timu uwanjani.
Inawezekana mfumo wa kuwalea vijana wetu tangu utoto katika soka ni jambo linalowaangusha, lakini wazawa wanapaswa kujiongeza kwa kujituma, kujielewa na kutambua soka ni ajira na sio sehemu ya burudani tu!
Kama wachezaji 510 wanashindwa kuibuka miongoni mwao kuwa nyota wa kupapatikiwa na makocha kwa ajili ya kuzitumikia timu za taifa na hata kutakiwa nje ya nchi, hapo nani wa kulaumiwa?
Ukifuatilia kikosi cha Stars kwa miaka ya karibuni wanaounda ni wachezaji wa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam na kidogo Mtibwa Sugar?
Ila kwa wanaokumbuka zamani, Stars ilikuwa ikiundwa na wachezaji kutokana klabu kubwa na zile za mikoani ambazo zilikuwa na timu zenye majembe ya maana wanaowatoa jasho mastaa wa Simba na Yanga, kwanini leo inashindana? Tujiulize!
TUJIFUNZE KWA WENZETU
Madai kuwa nyota wa kigeni ni chanzo cha kukwama kwa wazawa na kuikwamisha timu ya taifa, kwa kuiangalia DR Congo tunaweza kujifunza kitu. DR Congo ambayo kwa sasa ipo Fainali za Afcon ni moja ya nchi yenye kupokea nyota wa kigeni wanaokipiga TP Mazembe, AS Vita, DC Motema Pembe, FC Lupopo na nyingine, lakini kimataifa The Leopards inakimbiza mno!
Kwa msimu uliopita ambao TP Mazembe iliitoa Simba kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa na nyota 13 wa kigeni kati ya wachezaji 30 ilionao.
Hata hivyo, DR Congo imekuwa na mafanikio kisoka katika anga la kimataifa ikiwa na rekodi ya kubeba taji ya Afcon mara mbili katika ushiriki wao wa mara 19, huku ikishika nafasi ya tatu mara mbili, nafasi ya nne mara moja.
Pia ikumbukwe DR Congo ilifika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1974 huku klabu zake za Mazembe na AS Vita zikinyakua mara kadhaa mataji ya Afrika ama kufika hatua za juu za michuano ya CAF kwa kutegemea muunganiko wa wazawa na wageni.
NINI KIFANYIKE
Ili kwenda na kasi ya wageni na kuisaidia Taifa Stars kuwa imara ni lazima wachezaji waongeze kiu ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania. Taifa Stars leo inamtegemea Mbwana Samatta, Simon Msuva, Shaaban Idd Chilunda, Farid Mussa, Hassan Kessy, Thomas Ulimwengu, Rashid Mandawa, Adi Yusuf na wengine. Uwepo wa wachezaji hawa umekuwa ukiongeza kitu tofauti ndani ya Stars kutokana na kuwa na uzoefu na soka la kulipwa.
Kama tutaendelea kusubiri kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Mwinyi Haji Mngwali, Said Dilunga na wengine kuendelea kutengewa nafasi za upendeleo klabuni basi na Stars nayo tutasubiri sana. Soka ni mchezo wa hadharani na msingi wake ni nidhamu na kujituma huku ukifuata maelekezo ya mwalimu, kutaka kupiganiwa ili upate nafasi za upendeleo ni kujidanganya. Lakini, wachezaji wetu wapambane kuwania namba.