Mbeya yasuka mipango ya kurejesha nne Bara

Muktasari:
- Mbeya ilikuwa ikichuana na Dar es Salaam kwa kuwa na idadi kubwa ya timu nyingi Ligi Kuu, ambapo msimu wa 2021/22 ilikuwa nazo nne zikiwamo, Ihefu, Mbeya Kwanza, Tanzania Prisons na Mbeya City.
CHAMA cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa) kimesema kupoteza timu tatu zilizokuwa Ligi Kuu si jambo la kufumbia macho, bali inahitaji mkakati wa pamoja kurejesha heshima ya mkoa huo.
Mbeya ilikuwa ikichuana na Dar es Salaam kwa kuwa na idadi kubwa ya timu nyingi Ligi Kuu, ambapo msimu wa 2021/22 ilikuwa nazo nne zikiwamo, Ihefu, Mbeya Kwanza, Tanzania Prisons na Mbeya City.
Hata hivyo, baada ya msimu huo, Mbeya Kwanza ilishuka daraja, huku msimu uliofuata Ihefu ikapotea kabla ya kupigwa mnada msimu uliopita kuwa Singiga Black Stars, huku KenGold ikipanda na kushuka tena.
Hadi sasa Mbeya imebaki na timu moja ya TZ Prisons, inayopambana kukwepa kushuka daraja kutokana matokeo iliyonayo, huku Mbeya City ikipanda Ligi Kuu msimu ujao.
Mwenyekiti wa chama hicho, Elias Mwanjala amesema kushuka kwa timu hizo, kunawahitaji wadau, viongozi na Mrefa kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kurejesha heshima.
Alisema kabla ya kuondoka madarakani, Mbeya ilikuwa ikichuana na Dar es Salaam kwa kuwa na idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu, lakini kwa sasa inatia aibu kwa mkoa huo wenye uchumi na vipaji kuwa na timu chache.
“Inahitaji nguvu ya pamoja na sisi Mrefa tutapambana kuwakutanisha wadau na viongozi wa timu tujadili kwa pamoja namna ya kurejesha hizi timu na kufufua heshima yetu,” alisema Mwanjala.
Leonard Mwakyenda mdau wa soka jijini Mbeya, alisema njia bora ya kurejesha timu zilizoshuka daraja ni kutafuta wadau wenye uwezo kiuchumi kusapoti timu hizo akieleza kuwa mpira wa sasa ni pesa.
“Kwa kuwa Mrefa ina viongozi wenye nia na mapenzi ya mpira na wanajitolea, hili linawezekana, kimsingi viongozi wa hizi timu wawe tayari kutoa ushirikiano, Mbeya ina vipaji na watu wanapenda mpira,” alisema Mwakyenda.