Mbeya City yawageukia madogo

> Mbeya City
Muktasari:
Timu hiyo juzi Jumamosi ilifanya kliniki maalumu ya soka kwa vijana wadogo wenye umri kati ya miaka 8-15 kwenye uwanja wa FFU jijini Mbeya kwa lengo la kutafuta wachezaji wa kupandisha kwenye timu ya vijana.
BAADA ya kuondokewa na mastaa wengi wa kikosi cha kwanza waliokimbilia Simba, Yanga na Mwadui, Mbeya City imepata ujanja mpya wa kutengeneza wachezaji kwenye timu ya vijana ambao watakuwa hazina siku zijazo.
Timu hiyo juzi Jumamosi ilifanya kliniki maalumu ya soka kwa vijana wadogo wenye umri kati ya miaka 8-15 kwenye uwanja wa FFU jijini Mbeya kwa lengo la kutafuta wachezaji wa kupandisha kwenye timu ya vijana.
Kocha Mohammed Kijuso alisema: “Nimefurahishwa na vipaji vingi nilivyoviona, hii inaonyesha kuwa vijana wengi wanataka kucheza mpira. Jambo hili ni endelevu na nina uhakika tutaibua vipaji vingi ambavyo vitakuwa manufaa kwa Mbeya City kwa miaka ijayo.”
Kliniki hiyo yenye lengo la kusaka vipaji ambavyo vitaingizwa moja kwa moja kwenye timu za vijana ilikuwa chini ya usimamizi wa makocha Mohamed Kijuso na Rashid Kasiga.
Kijuso pia alisema kuwa anafahamu lengo la Mbeya City kuanzisha kliniki hiyo ilikuwa ni kuhakikisha wanatengeneza timu nzuri ya baadaye.“Lengo la klabu yetu ni kuwa na timu imara za vijana, na hata timu ya wakubwa ili timu isiweze kusumbuka kwenye kusajili,” alisema.