Mbeya City yamnyatia nyota wa Yanga

Muktasari:
- Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti, Farid ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na kikosi hicho kitakachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao, kwa lengo la kukiboresha kwa kushirikiana na nyota wengine watakaojiunga nao.
UONGOZI wa Mbeya City umeanza hesabu za kuiwinda saini ya winga wa Yanga, Farid Mussa ili kuongeza nguvu ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, ikiwa ni katika harakati za kukisuka kikosi hicho ili kilete ushindani zaidi.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti, Farid ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na kikosi hicho kitakachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao, kwa lengo la kukiboresha kwa kushirikiana na nyota wengine watakaojiunga nao.
“Ni kweli Farid yupo katika mipango ya Mbeya City na kama kila kitu kitaenda sawa basi tunaweza kukamilisha uhamisho huo mapema iwezekanavyo, ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu tunayeamini atatusaidia huko mbele,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City (CEO), Ally Nnunduma alisema tayari mipango ya kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao imeanza, ingawa ni mapema sana kuweka wazi ni mchezaji gani wanayemuhitaji ili kuongeza nguvu zaidi.
“Nafikiri baada ya Ligi Kuu kuisha tutakuwa na wigo mpana wa kuzungumza ni nani tunayemuhitaji, ila kwa sasa nikuombe tu uwe na subra kwa sababu kinachoendelea ni vikao vya ndani kati yetu uongozi na benchi letu la ufundi,” alisema Ally.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua, Farid mkataba wake unaisha mwakani 2026 na viongozi wa Mbeya City wanahitaji kuipata saini yake ya moja kwa moja, ingawa kama itashindikana pia basi wapo tayari kumpata kwa mkopo ili kuongeza uzoefu wake.
Farid ni miongoni mwa wachezaji wazawa wenye vipaji vikubwa huku akichezea timu mbalimbali, zikiwamo za Azam FC, kabla ya kutimkia CD Tenerife B ya Hispania, kisha kurejea nchini na kujiunga rasmi na kikosi cha Yanga, Agosti 12, 2020.
Mbeya City inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa FC, ameirejesha tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, huku kocha huyo akiweka rekodi ya kuipandisha timu kwa mara yake ya pili.
Kwa mara ya kwanza, kocha huyo aliipandisha JKT Tanzania msimu wa 2022-2023, baada ya kikosi hicho cha maafande kumaliza mabingwa kwa pointi 63, kikiungana na Kitayosce kwa sasa Tabora United iliyomaliza ya pili, kufuatia kufikisha pointi 60.
Mbeya City imemaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 68, baada ya kushinda mechi 20, sare nane na kupoteza mbili, nyuma ya Mtibwa Sugar iliyoibuka bingwa mpya msimu huu, kwa kumaliza kileleni mwa msimamo ikiwa pointi zake 71.