Mbeya City yajifungia saa tatu Sokoine, Lule ni pasi moja bao

Muktasari:

  • Mbeya City inawakaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Jumatatu kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mbeya. Mbeya City imeendelea kujiweka fiti kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, baada ya leo Jumamosi kutumia zaidi ya masaa mawili huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mathias Lule akielekeza nguvu kwenye pumzi, pasi na kufunga mabao.

Timu hiyo inatarajia kuwa uwanjani Jumatatu kuwakaribisha Wekundu hao, mchezo utakaopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Katika matizi ya leo yaliyofanyika uwanjani hapo yalidumu kwa masaa matatu huku Lule akionekana kuwa siliasi na vijana wake kutimiza majukumu yao.

Kocha huyo raia wa Uganda pamoja na mazoezi mengine, lakini alijikita zaidi kuwapa matizi ya viungo, kukaba, kupiga pasi, lakini kubwa ikiwa ni kufunga mabao.

Hata hivyo wachezaji hao hawakumuangusha ambapo mitihani yote walionekana kuishinda, huku Winga wake, Helbet Lukindo aking'ara zaidi kwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Lule amesema amefurahishwa na kile walichofanya nyota wake na kwamba huenda wakafanikisha malengo yao Jumatatu.

"Hadi sasa sina majeruhi yeyote anayeweza kukosa mechi kwa wale ninaotarajia kuwatumia katika mchezo ujao na kwa kile walichofanya leo huenda tukafanikisha malengo" amesema Lule.

Hata hivyo katika mazoezi hayo, makomandoo walikuwa makini kutoruhusu shabiki yeyote kuingia uwanjani wakieleza kuwa ni maelekezo kutoka juu.