Mbeya City yaitangazia vita Simba

Monday June 21 2021
mbeya city pic
By Mwandishi Wetu

SIMBA juzi walikuwa jijini Mwanza wakimalizana na Polisi Tanzania, kabla ya kuanza safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kujiandaa kuvaana na Mbeya City, iliyowapiga mkwara kwamba wajiandae kupata aibu nyumbani kwenye mechi yao itakayopigwa kesho Jumanne saa 1 usiku.

Tambo hizo za Wagonga Nyundo hao wa Green City, imetokana na kuendeleza moto wao ndani ya duru la pili, ambapo juzi walitoka kuinyoosha Coastal Union kwa mabao 2-0 na kufufua matumaini ya kusalia kwenye Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Mabao ya Juma Liuzio na lile la George Sangija yaliipa ushindi muhimu Mbeya na wakidai hata Simba ikizubaa wajue nao watakaa, kwa vile wamepania kumaliza mechi zao za kufungia msimu kibabe..

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe, alisema baada ya kumalizana na Coastal kwa sasa nguvu zao zote ni kuelekea kwenye mechi ijayo dhidi ya Simba.

“Tunaenda kucheza na timu bora katika ligi, lakini hilo kwetu halitutishi tuko tayari kupambana mpaka tone la mwisho,” alisema Kimbe akisisitiza benchi lao la ufundi na wachezaji wamemhakikishia Kwa Mkapa, patachimbika.

Hata hivyo rekodi zinaonyesha katika mechi zao nne zilizopita za Ligi Kuu, Mbeya imechapika zote nje ndani, hivyo kutakiwa kugangamala kweli kama wanataka kuizuia Simba isifanye yao ikiendelea kusaka taji la nne mfululizo. wa michuno hiyo.

Advertisement


IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI

Advertisement