Mbeya City, Simba liwalo na liwe

Summary

  • Katika mechi 14 walizokutana Simba imeshinda 12, sare moja na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 29 kati ya 35 yaliyofungwa.

Mbeya. Wakati mechi ya Mbeya City na Simba ikisubiriwa kwa hamu, mashabiki wa timu hizo wametunishiana msuli kila upande ukitamba chama lake kushinda.

Timu hizo zinakutana ikiwa kila upande unajivunia rekodi yake tangu zianze kukutana msimu wa 2014/2015.

Hadi sasa timu hizo zimekutana mechi 14, ambapo Simba ameshinda 12, sare moja na kupoteza moja.

Wenyeji Mbeya City licha ya kuchezea vipigo vingi, lakini inavimba kutokana na msimu uliopita kuilaza Simba bao 1-0 katika uwanja wa Sokoine.

Hata hivyo Straika na nahodha wa Wekundu, John Bocco ndiye mchezaji aliyeifunga sana City akiwa amewanyoosha mabao 13.

Pia Simba imefunga mabao mengi dhidi ya wapinzani hao, kwani kati ya 35 yaliyofungwa kwenye mechi hizo 14, Wekundu wameingia wavuni mara 25 kwa sita.

Mwenyewe wa matawi ya Simba mkoani Mbeya, Abel Edson amesema wa leo wanahitaji ushindi ili kukaa kileleni, akieleza kuwa siku saba walizotumia kulinda uwanja lazima wafanye kweli.

"Leo hakuna cha mwenyeji hapa, tunajua tunacheza na Mkoa na timu nyingine zilizoipa nguvu Mbeya City, kila mmoja ashinde mechi zake" amesema Edson.

Naye Yusuph Mwangete shabiki wa Simba tawi la Soweto amesema wanaamini leo kushinda na kwamba wanasubiri uamuzi wa kocha Juma Mgunda atakayempanga atafunga mabao.

"Nia yetu Simba ni kutwaa ubingwa hivyo Mbeya City watusamehe hatuchezi nao, hii ni miongoni mwa timu tunazopaswa kufunga" amesema Mwangete.

Shabiki wa Mbeya City Olongile Nchesa amesema timu leo wanatarajia pia ushindi akibainisha kuwa hata msimu uliopita haikuwa bahati mbaya kuwafunga Simba.

"Na tunawafunga mbili, tuna timu bora msimu huu na timu nyingi zinatukamia sana, angalia mechi zilizopita lakini tumepambana" ametamba shabiki huyo.