Mbeya City mdogo mdogo hadi kieleweke, yawakanda Maafande

Mbeya. Mbeya City haipoi na haiboi kutokana na maendelezo wake mzuri kwenye Championship kwa kushinda mechi mbili mfululizo na kukwea tena kileleni katika msimamo wa ligi hiyo.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita kupitia play off kwa kufungwa Mashujaa iliyokuwa Championship inapambana kurejea tena Ligi Kuu.

Katika mechi ya kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Green Warriors na leo ikatakata 2-0 dhidi ya Transit Camp, mechi zote ikitumia uwanja wake wa Sokoine jijini hapa.


Zifuatazo ni dondoo za mechi hiyo

City inarejea kileleni kwa pointi sita sawa na Pamba Jiji FC ya Mwanza lakini ikinufaika kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga (saba) na kufungwa matatu.

Straika wa timu hiyo, Maulid Shaban anafikisha mechi mbili akifunga mfululizo mabao mawili kila mchezo na kufikia manne na kuwa kinara wa mabao hadi sasa kwenye championship.

Transit Camp inaondoka uwanja wa Sokoine Mbeya kwa pointi moja kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Ken Gold na kuruhusu wavu wao kuguswa mara tatu ikifunga moja katika michezo miwili.

Katika mabao ya leo yamepatikana kwa penalti kutokana na sababu tofauti ikiwa ni kushika mpira eneo la hatari kwa beki wa Transit Camp na kuchezewa rafu mchezaji wa Mbeya City.

Mchezo ujao City itakuwa ugenini kuwafuata ndugu zao Mbeya Kwanza mechi itakayopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara walipohamishia makao yao ya muda, huku Transit Camp ikiwa nyumbani dhidi ya Faountain Gate.