Mbelwa nusura avunje pua Namibia

Muktasari:

  • Kilichomkuta, bondia huyo anakwambia alipigwa panchi ya kulia ya nguvu ambayo hatokaa akaisahau kwenye maisha yake ya ngumi kwani alihisi kama amecharangwa mapanga mwili mzima.

UMEWAHI kusikia bondia wa uzito wa juu (heavy weight) anazichapa na yule wa uzani wa kati (middle weight)?, hiyo ilimkuta bondia wa Bongo, Said Mbelwa ambaye anakwambia nusura anyofolewe pua na konde lililomzidi uzito kisa kucheza pambano lisilomhusu.

Mbelwa anakwambia alivunjwa mwamba wa pua kwenye pambano hilo ambalo awali lilikuwa aende kucheza na bondia wa uzito wa juu Nchini, Alphonce Mchumiatumbo lakini akapelekwa dakika za mwisho mwisho.

“Ilikuwa nchini Namibia, tulipopima mpinzani wangu alikuwa na kilogramu 90 mimi nilikuwa na 79 lakini nikacheza hivyo hivyo kwani pambano lile lilikuwa la uzito wa juu na alipaswa aende Mchumiatumbo, lakini alipoteza sifa za kucheza baada ya kupigwa KO siku chache kabla ya kwenda Namibia.

“Kilichotokea nikapewa mchongo niende kucheza kule na dau langu nikapewa kabisa, wala sikuona tatizo licha ya kwamba mpinzani wangu alinizidi kilo 11, nikaridhia kwenda kupigana hivyo hivyo” anasema Mbelwa.

Kilichomkuta, bondia huyo anakwambia alipigwa panchi ya kulia ya nguvu ambayo hatokaa akaisahau kwenye maisha yake ya ngumi kwani alihisi kama amecharangwa mapanga mwili mzima.

“Ile ngumi ilinivunja mwamba wa pua, muda ule ulingoni nilihisi maumivu ya kawaida tu, lakini baada ya masaa mawili, maumivu niliyoyasikia hayaelezeki.”