Mbao FC yachapwa Ligi Daraja la Kwanza

Dar es Salaam. Hali imekuwa tete kwa timu zilizoshuka Ligi Kuu huko kwenye Daraja la Kwanza (FDL) baada ya juzi Mbao FC nayo kuchezea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Rhino Rangers.

Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na kuishuhudia timu hiyo ikianza vibaya kwa mabao yaliyofungwa na Hamis Thabit na Shija Mongo huku lile la kufutia machozi kwa upande wao likifungwa na Daniel Boniface.

Ilianza Alliance FC kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, kisha Singida United ikalala 2-0 kwa Geita Gold, Ndanda FC ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na African Lyon huku Lipuli FC ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Mawenzi Market.

Timu hizo zilishuka msimu uliopita baada ya Alliance kumaliza ligi ikiwa mkiani huku Ndanda, Lipuli na Singida United zikishuka moja kwa moja.

Mbao FC ilishuka baada ya kushindwa kufanya vizuri dhidi ya Ihefu SC iliyokuwa FDL katika michezo yao ya mwisho hatua ya mtoano ambayo Ihefu ilinufaika kwa mabao ya ugenini.

Licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Rhino Rangers, Kocha wa Mbao FC, Almas Moshi alisema vijana wake walipambana isipokuwa haikuwa bahati yao kuondoka na alama tatu.

Aliongeza kuwa pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini hawawezi kukata tamaa isipokuwa wanajipanga upya kurekebisha makosa na kupata ushindi kwenye michezo inayofuata. “Vijana walipambana kadri ya uwezo wao na walitengeneza nafasi nyingi, hivyo tumeona makosa yetu tutaenda kuyarekebisha kuhakikisha tunashinda mechi zinazofuata,” alisema Moshi.

Mbao imepangwa kundi B pamoja na Alliance, Fountain Gate, Kitayosce FC, Transit Camp, Geita Gold, Singida United, Pamba FC, Rhino Rangers na Arusha FC.