Mawakili FC wakubali unyonge kwa Mahakama Moro

Muktasari:
- Uongozi wa kituo cha haki jumuishi Morogoro katika mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro imezindua maadhimisho ya wiki ya sheria kwa michezo mbalimbali huku ikitarajia kutoa elimu ya sheria kabla ya kufikia kidede cha maadhimisho hayo Februari 2 mwaka huu kwa kushirikiana na wadau.
MOROGORO. Timu ya Mahakama FC imetwaa ubingwa wa soka katika bonanza la michezo na mbio za marathoni kwa kuichapa Mawakili FC kwa bao 2-0 katika mchezo mkali wa fainali huku Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro akitamba katika mbio za kufukuza kuku Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Michezo hiyo ni ishara ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria kwa Mahakama ya Tanzania kanda ya Morogoro kwa kushirikisha wadau wa sheria kushiriki michezo mbalimbali na washindwa wakitunukiwa vyeti.
Akizungumza baada ya ushindi huo uwanjani hapo, mfungaji wa mabao yote ya washindi hao, Simon Fanuel alisema amefurahishwa kufunga mabao mawili pekee yake yaliyopelekea timu yake kuibuka kidedea na kutwaa ubingwa katika michezo hiyo kwa kuitandika wapinzani wao Mawakili Fc.
Fanuel alisema haikuwa kazi rahisi wao kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao japo walilazimika kutuliza akili na kutegua mbinu zao na kufanikisha kuwafunga bao mbili na kuzima ndoto za wapipinzani.
“Tulicheza kama timu ndio sababu tumeibuka na ushindi huu wa bao mbili lakini safu yetu ya ulinzi ilifanyka kazi kubwa ya kuzima mashambulizi ya wapinzani wetu hatimaye Mahakama Fc tumekuwa na furaha baada ya dakika 90 na kutwaa ubingwa wa bonanza la michezo na mbio za marathoni uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria kwa Mahakama ya Tanzania kanda ya Morogoro.” alisema Fanuel.
Katika mchezo wa Netiboli, Mahakama iliigeza mdebwedo timu ya Chama cha wanasheria sheria Tanganyika (TLC) kwa kuilaza kwa vikapu 15-1, huku katika mbio za riadha za kilometa tano, Bonifasi Masubo akishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa dakika 26 wakati, Amina Mranda akishinda kwa upande wa wanawake kilometa tano kwa kumaliza dakika 32.
Sajenti wa jeshi la polisi Morogoro, Fredy Afyukile alitamba katika mchezo wa drafti kufuatia kukusanya pointi tisa na kutawazwa mshindi wakati Hamis Kibwana akitangaza ufalme katika mchezo wa bao kwa kutawa ubingwa huo kwa kuwa na pointi nane kwa upande wa karata, Richard Moses akiibuka kinara na Nansi Samuel akiwa kidedea kwa wanawake.
Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro, Paul Ngwembe aliibuka mshindi katika mbio za kufukuza kuku akiwazidi maarifa wapinzani wake nane na kuondoka na kitoweo hicho nyumbani wakati wanawake, Kidawa Mohemad akitamba katika mbio kwa kukamata kuku.
Mchezo wa magunia, Mustapha Sultan alishinda mbio hizo za mita 50 na Mkaleso Nyange akiibuka kwa akinadada na kamba mahakama iliitabia TLC kwa ushindi wa 2-0 wanaume na wanawake.